30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

KEYDOLI; MREMBO KUTOKA KENYA AMWAGIA SIFA HARMONIZE

MOMBASA, KENYA 

ONGEZEKO la wasanii wapya halipo Bongo pekee bali mpaka nchini Kenya, mashabiki wameendelea kushuhudia vipaji vipya kila siku. 

Swaggaz tumekutana na KeyDoli, mrembo kutoka Mombasa nchini Kenya anayefanya vyema kwa sasa na wimbo, Infinity aliomshirikisha rapa Country Boy akitumia staili ya Afro Arabic Soul. 

Swaggaz: KeyDoli ni nani na lini ulianza kujihusisha na muziki? 

KeyDoli: Jina langu halisi ni Yusriyah Ahawa, nilianza muziki nikiwa mdogo sana kama miaka 14 hivi, ilikuwa mwaka 2002. 

Nilipata kutambulishwa na prodyuza mmoja anayeitwa Bruce Othiambo ambaye alikuwa rafiki wa baba yangu kwa sababu walikuwa wanafanya kazi sehemu moja. 

Prodyuza Bruce ambaye sasa ni marehemu alikuwa kwenye studio zinaitwa Johari Cleff na ndio ilikuwa inasimamia wasanii wakubwa kutoka Kenya. 

Ngoma yangu ya kwanza iliitwa Nipe na baba yangu ndio alirekodi akishirikiana na prodyuza Bruce, wimbo huo ulinipa umaarufu sio tu hapa Kenya bali na Afrika Mashariki na Uingereza. 

Swaggaz: Wanamuziki gani walikuvutia mpaka ukaingia kwenye muziki? 

KeyDoli: Nilizaliwa kwenye familia ya muziki ndiyo maana nikajikuta napenda kuimba kwa kuwa hata baba yangu alikuwa anapenda muziki. 

Nikawa nasikiliza muziki wa Yondo Sister, Mbilia Bel na Franco huku Madonna akiwa ni msanii wangu pendwa na haipiti siku sijamsikiliza. 

Swaggaz: Kwanini uliamua kutangaza muziki wako Tanzania kwa kumshirikisha rapa Country Boy? 

KeyDoli: Toka zamani ilikuwa ndoto yangu nifike Tanzania. Kwa hadithi za mama aliniambia amezaliwa Bongo pia nilikuwa nikiwasikia kina Juma Nature, Lady Jay Dee na Ray C kwahiyo nilikuwa natamani nifike. 

Nilitamani kufika Tanzania nikiwa mdogo ila kwa sababu nilikuwa shule nilishindwa lakini nashukuru Machi 1, mwaka huu nilifika Dar es Salaam na kuweza kutimiza ndoto yangu kufanya kazi na Country Boy. 

Swaggaz: Ukiwa kama msanii wa kike na mrembo sana, changamoto zipi unapitia kwenye muziki wako? 

KeyDoli: Sio rahisi ila mimi nilifunzwa toka nikiwa mdogo kuwa wakati wa biashara ni biashara tu, ukiwa na mazungumzo ya biashara hakuna mtu anaweza kukutongoza ndio maana nikiwa nakwenda kwenye studio kurekodi au redioni au kwenye Tv huwa nakuwa na mtu kando yangu ili kukwepa hizo changamoto. 

Swaggaz: Mbali na Country Boy, wasanii gani wengine wa Tanzania unatamani kufanya nao kazi? 

KeyDoli: Harmonize au Darassa lakini Harmonize zaidi maana mashallah yuko na moyo mweupe na nilipata bahati ya kumwona hana dharau wala kiburi na uimbaji wake ni mzuri pia Darassa navutiwa na floo zake. 

Swaggaz: Changamoto zipi zipo kwenye tasnia ya muziki hapa Kenya? 

KeyDoli: Mimi naona sapoti hamna sana lakini siwezi kulaumu vyombo vya habari kwa sababu kuna wengine hawajafikishiwa kazi pia mashabiki nao hawajafikishiwa muziki kwa usahihi ili waweze kuusapoti. 

Swaggaz: Baada ya kuachia ngoma yako na Country Boy, mashabiki watarajie nini kutoka kwako? 

KeyDoli: Niko na ngoma mpya nitaiachia Mei 21, mwaka huu nikiwa nimemshirikisha msanii mkubwa wa Tanzania. Huo wimbo upo kwenye albamu yangu yenye jumla ya nyimbo 12. 

Pia niko na EP yenye nyimbo nne ambazo zote nimeshirikisha Country Boy na tayari zina video ambazo nilifanyia Tanzania. 

Mashabiki waendelee kunitafuta kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, YouTube naitwa Keydoli ili wapate kunifahamu zaidi nawapenda sana Watanzania. 

Pia nawakumbusha tuendelee kuvaa barakoa na kunawa mikono na kutumia sanitaiza mara kwa mara ili Mungu atulinde na ugonjwa wa corona. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles