DAMIAN MASYENENE, MWANZA
WAKATI Yanga ikishuka dimbani kuikabili Kagera Sugar leo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera, amebuni mikakati mipya ya kuvuna pointi tatu kwenye michezo yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosalia.
Timu hizo zitaumana katika pambano litakalopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, ambao miamba hiyo yenye makao yake makuu Jangwani jijini Dar es Salaam, inautumia kama uwanja wake wa nyumbani.
Yanga inautumia uwanja huo kama uwanja wake wa nyumbani, baada ya Uwanja wa Taifa kupangwa kutumika kwa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17(Afcon-U17).
Akizungumza na MTANZANIA, Zahera alitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuwadhibiti wachezaji wake wasizurure huku akiwasisitiza kulala mapema.
Pia alisema kutokana na wachezaji wake kucheza mechi nyingi mfululizo, hahitaji kuwafanyisha mazoezi magumu.
“Hatuna muda wa kufanya mazoezi magumu zaidi, huwa nawakumbusha mambo muhimu kwa kufanya vikao na wachezaji waandamizi ambao watafikisha ujumbe kiurahisi kwa wenzao umuhimu wa kila mchezo,” alisema Zahera.
Zahera alisema ataikabili Kagera akifahamu ni timu ngumu kufungika, hivyo ameamua kudhibiti tabia za wachezaji ikiwemo kuchelewa kulala na kuzunguka hotelini usiku wakati timu ina mchezo.
“Kuna wachezaji wanaitwa viongozi kufuatana na programu, unajua tunacheza mechi nyingi za kufuatana, ile meseji nawapatia wachezaji, hata jana tumefanya kikao usiku na wachezaji wote.
“Alafu mwisho nawaita tena wale viongozi, wenyewe watapeleka tena meseji kwa wenzao, watakaa nao na kuwaeleza kwamba tuna na mechi na Kagera, hivyo hatupendi kuona mchezaji saa tatu awe kwenye korido, inatakiwa kila mtu awe chumbani kwake apumzike alale vizuri,” alisema.
Ubingwa
Zahera amesisitiza bado wako kwenye mbio za ubingwa na njia ya kutwaa taji hilo iko wazi kwao, endapo tu mamlaka husika hazitoweka ujanja ujanja ukiwemo upangaji wa ratiba.
“Kama ligi itachezeka vizuri na mipango inakwenda vizuri kwa timu zote, basi hatuna tatizo na ubingwa, lakini haya mambo yanayoendelea ndio yanatutia wasiwasi, viporo si shida lakini kuwe na haki na utaratibu mzuri, wala hatuna hofu na ubingwa.
“Matokeo yetu yanaonyesha wazi kuwa ni timu inayofaa kubeba ubingwa, lakini haya mambo mengine yanayofanyika ndiyo yanachafua kila kitu,” alisema Zahera.
Yondani arejea
Baada ya kushindwa kuumaliza mchezo uliopita dhidi ya African Lyon kutokana na kuumia goti, beki Kelvin Yondan leo atakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kitakachoikabili Kagera.
“Mechi ya jana (Jumatatu) alitoka baaada ya kugongwa goti, nikaona nimpumzishe ajiandae kwa mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao, kwa hiyo anaweza kutumika leo tutaona,” alisema.
Kwa upande mwingine, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, anaamini kikosi chake kina fursa ya kulipa kisasi dhidi ya Wanajangwani hao.
Mexime alisema wamepania kushinda mchezo huo ili kuvuna pointi tatu na kusogea juu ya msimamo wa ligi na kujiweka mbali na msimamo wa ligi.
Hata hivyo, alikiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na mwendelezo wa matokeo yao mabaya kwenye ligi hiyo, wakitoka kupoteza michezo miwili mfululizo, baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Azam FC kisha kutunguliwa mabao 2-1 na Singida United.
“Mchezo utakuwa mgumu lakini tunaweza kuumudu na kupata ushindi baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu uliopita, wachezaji tuliokuja nao wako fiti na kikosi chote kimekamilika.
“Bado ni mechi ngumu kwetu lakini tumekuja kupambana ili tupate matokeo ya ushindi kwa sababu hali yetu kwenye msimamo wa ligi si ya kujivunia,” alisema Mexime.
Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Novemba 25, mwaka jana kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera Sugar ililala mabao 2-1.
Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 71 baada ya kushuka dimbani mara 30, ikishinda 22, sare tano na kupoteza michezo mitatu.
Kagera yenyewe inakamata nafasi ya 17 miongoni mwa timu 20 zinazoshiriki ligi hiyo, ikiwa na pointi 36 ilizozipata baada ya kucheza michezo 31, ikishinda nane, sare 12 na kupoteza michezo 11.