22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yajivinjari kileleni

NA SALMA JUMA, TANGA
USHINDI wa bao 1-0 dhidi ya Wagosi wa Kaya wa Tanga, timu ya Coastal Union jana umeifanya Yanga kujivinjari kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 22 katika msimamo wa ligi hiyo.
Yanga imejikusanyia pointi hizo baada ya kucheza michezo 12, huku ikibakiza mechi yake ya kiporo dhidi ya Mbeya City, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 21 huku ikiwa imecheza michezo 11, Mtibwa inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 18.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa, Yanga walipata bao lao la kwanza dakika ya 11 kupitia kwa nahodha wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyeunganisha nyavuni kwa kichwa mpira uliorushwa na beki wa pembeni, Mbuyu Twite.
Bao hilo lilitokana na makosa ya kiungo wa Coastal, Abdulhalid Humud kuleta uvivu na kushindwa kuruka kuucheza mpira huo wa kurushwa, ambapo ulimkuta mfungaji.

Timu zote zilianza kipindi cha kwanza kwa kushambuliana kwa zamu, lakini walikuwa ni Coastal Union walioanza kulifikia lango la wapinzani wao kwa dakika ya tano kutokea piga ni kupige kwenye goli la Yanga, ambapo mabeki wake waliokoa hatari hiyo.
Kipa wa Coastal, Shaaban Kado katika dakika ya tisa alifanya kazi ya ziada kuokoa hatari iliyoelekezwa langoni mwake, kutokana na mpira wa adhabu uliyopigwa na Mbrazil, Andrey Coutinho lakini pia hali kama hiyo ilimkuta kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’, ambaye alifanya naye kazi ya ziada kuokoa shuti kali la Humud.
Mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, Amis Tambwe, ambaye hadi sasa bado hajafanya makubwa tangu atue Jangwani, alikosa bao la wazi dakika ya 45 baada ya shuti lake kutoka nje ya lango la Coastal.
Mwamuzi wa mchezo huo, Athman Lazzi kutoka Morogoro aliyekuwa akisaidiwa na Rashid Zongo wa Iringa na Isihaka Shirikisho wa Tanga, alimwonyesha kadi ya njano Coutinho baada ya kubishana na mwamuzi na Hussein Swed pia kwa kosa hilo hilo.
Yanga inatarajia kushuka tena dimbani Jumapili hii kuvaana na Mtibwa, mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini tayari wana Jangwani hao walishaomba Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) liahirishe mchezo huo.
Nia ya Yanga kuomba kuahirishwa mchezo huo ni kutaka kupata nafasi nzuri ya kujiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya BDF IX ya Botswana, ambapo wataanzia nyumbani.

Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Juma, Simon Msuva, Salum Telela, Amis Tambwe/Danny Mrwanda, Kpah Sherman na Andrey Coutinho/Hussein Javu dk65.
Coastal: Shaaban Kado, Hamis Mbwana, Sabri Rashid, Abdallah Mfuko, Juma Lui, Abdulhalim Humud, Joseph Mahundi/Mohammed Mtindi dk66, Godfrey Wambura, Hussein Swed, Rama Salim na Hubu Imbem.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles