24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Kikwete awatolea uvivu Takukuru, DPP

rais-kikweteNa Kulwa Mzee, Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete ameijia juu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Jeshi la Polisi kwa kusema kuwa wana viherehere vya kukurupuka, kuwakamata watu na kuwafikisha mahakamani bila ushahidi unaojitosheleza.

Rais Kikwete alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya Sheria ikiwa ni mara yake ya nane na ya mwisho kuhudhuria hafla hiyo akiwa kiongozi wa nchi.

Alisema ofisi ya DPP, Polisi wapelelezi na Takukuru hawatakiwi kuwa chanzo cha kukwamisha kesi kuendelea mahakamani.

“Ofisi ya DPP, Takukuru na wapelelezi hata sijui wana kiherehere cha kitu gani, wanapeleka kesi mahakamani bila kukamilisha upelelezi, kama upelelezi haujakamilika msiwakamate watu, mnatafuta sifa za nini?

“Mnafikisha kesi mahakamani wakati upelelezi haujakamilika mwishowe mnawasilisha nini mnaita…Nole Prosecure, mimi sio mwanasheria.. mchumi, eti DPP anaondoa kesi mahakamani baada ya kuona hana haja ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa, baadaye hiyo kesi hairudishwi tena mahakamani.
“Mnakurupuka nalo jambo, mnaendesha upelelezi kwa kusikiliza maneno ya nje, si jambo zuri, jiandaeni sawasawa ufike wakati watuhumiwa watiwe hatianui, hiyo ndiyo heshima kwenu.

“Mfikisheni mtu mahakamani baada ya kuhakikisha kwamba kuna kesi, kumkamata mtu na kumwachia kwa nole ni kuwanyima haki,”alisema.

Rais Kikwete aliamuru mabaraza ya ardhi ya wilaya kuchukuliwa hatua kwa kukaidi amri ya Mahakama Kuu kupeleka majalada pale inapotokea kuna rufaa imekatwa.

“Mabaraza ya Ardhi hayatii amri ya Mahakama Kuu, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi iyachukulie hatua mabaraza yanayokaidi kupeleka majadala Mahakama Kuu pale yanapohitajika,”alisema.

Alikubaliana na hoja ya Jaji Mkuu, Mohammed Othman Chande ya kupanua wigo ili wananchi wasiokuwa na uwezo wa kuweka mawakili katika kesi wapate mawakili wa kuwatetea bure.

“Naikubali hoja ya Jaji Mkuu, Serikali italifanyia kazi ni wazo jema kugharimia huduma ya mawakili kwa wasiokuwa na fedha za kuweka wakili katika makosa makubwa nje na kesi za mauaji na yale yenye vifungo virefu, tupanue fursa ya wengi kupata haki,”alisema.
Alitoa rai kwa waendesha mashtaka, wapelelezi na mawakili wa kujitegemea kuunga mkono jitihada hizo kwani wao ni miongoni mwa wanaoweza kufanikisha hayo.

Aliahidi mwaka 2016 kila mkoa utakuwa na Mahakama Kuu yake kwani kufanya hivyo kutakuwa ni kusogeza huduma karibu na watu.

Jaji Chande alimpongeza Rais Kikwete kwa kuheshimu utawala wa sheria na uhuru wa mahakama katika kipindi chake chote cha uongozi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema utaratibu uwekwe na sheria ya mwenendo wa mashauri dhidi ya Serikali kuwa utekelezaji wa hukumu dhidi ya Serikali ufanywe kupitia kwa Katibu Mkuu Hazina.

Alisema jambo hilo limekuwa likitekelezwa japokuwa wakati mwingine malipo husika huchelewa kutolewa.

“Natambua kuwa kupitia mpango wa matokeo makubwa sasa utaratibu huo unaboreshwa ili kuwawezesha watu wanaoshinda kesi dhidi ya Serikali kupata haki mapema hasa pale ambapo hakuna rufaa iliyokatwa na Serikali.

“Kwa ujumla wajibu wa Serikali katika upatikanaji wa haki ni kuhakikisha kuna sheria zinazotoa haki kwa raia, uwepo muundo wa kitaasisi unaotosheleza kulinda haki na kutatua migogoro katika jamii, uwepo utaratibu mzuri unaoainisha namna watu wanakavyopata nafuu ya kisheria pale haki inapokiukwa,”alisema.

Masaju alisema Bunge lina nafasi yake katika upatikanaji wa haki nchini kwani ndicho chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria zikiwemo sheria zinazohusu haki na zile zinazoweka masharti kuhusu utaratibu wa kupata haki.

“Wabunge wamekuwa mstari wa mbele kufuatilia na kutaka kupata majibu kutoka kwa Serikali na Mahakama kuhusu wananchi ambao wamenyimwa haki zao.

“Hatua stahiki zimekuwa zikichukuliwa na Serikali na Mahakama kutokana na kilio cha wabunge kuhusu upatikanaji wa haki kwa wananchi hata hivyo Bunge linapaswa lifanye hivyo bila kuingilia mashauri yaliyoko mahakamani ili kuliepusha Bunge na tamaa ya kuingilia mihimili mingine ya dola, alisema Masaju.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles