22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yaipiga ‘mkono’ Majimaji

pg32 jan 22*Yarejea kileleni kwa kishindo, Tambwe apiga ‘hat trick’ ya pili

*Mwadui yachomoza kwa Kagera, Mtibwa yabanwa mbavu Mkwakwani

NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, walihitimisha mzunguko wa kwanza kileleni kwa kishindo baada ya kuifanyia mauaji timu ya Majimaji FC kwa kuishindilia mabao 5-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya Yanga kukabana koo na Azam FC kileleni wote wakiwa na pointi 39, Wanajangwani hao wanashika usukani kutokana na idadi nzuri ya wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Nyota wa mchezo katika mechi ya jana alikuwa mshambuliaji raia wa Burundi, Amissi Tambwe, aliyefanikiwa kuondoka na mpira baada ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ katika pambano hilo walilotawala.

Hiyo ilikuwa ni ‘hat trick’ ya pili kwa Tambwe msimu huu baada ya Disemba mwaka jana kupachika mabao matatu Yanga ikiilaza Stand United 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mabao matatu ya Tambwe yanamfanya kuongoza mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu kwani hadi sasa amefikisha mabao 13 huku akifuatiwa na Mganda, Hamis Kiiza, wa Simba aliyefunga mabao 10.

Yanga, wakicheza nyumbani, walianza kwa kasi ambapo dakika ya nne Thabani Kamusoko alifanikiwa kuandika bao la kuongoza akiunganisha vyema pasi ya winga Deus Kaseke.

Dakika ya 16 Kaseke akiwa katika nafasi nzuri alishindwa kuunganisha pasi safi ya Kamusoko na kuipatia timu yake bao, baada ya kupiga shuti hafifu lililodakwa kiulaini na kipa wa Majimaji, David Buruhan.

Kikosi cha Majimaji kinachoongozwa na kocha Kalimangonga Ongala, kilijitahidi kuonyesha soka safi na kujaribu bahati yao lakini mashuti ya mipira mirefu waliyokuwa wakiyaelekeza langoni kwa Yanga yalitoka nje.

Dakika ya 23 beki wa Yanga, Juma Abdul aliumia na kumlazimu kocha Hans van der Pluijm kufanya mabadiliko ambapo alimwingiza Said Juma, huku Majimaji wakimtoa Lulanga Mapunda aliyepata majeraha katika harakati za kuokoa mpira na nafasi yake kuchukuliwa na Kenned Kipepe.

Hata hivyo, Yanga walizidisha mashambulizi langoni kwa Majimaji na dakika ya 36 Msuva nusura aifungie bao la pili baada ya kuachia shuti kali akiwa ndani ya 18, lakini mpira uligonga mwamba na kutoka nje.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya 46 Mzimbabwe, Donald Ngoma alifanikiwa kufunga bao la pili akiunganisha pasi safi ya Kamusoko.

Dakika ya 54, Majimaji walikosa bao la wazi kupitia kwa Mapunda ambaye alipiga shuti kali langoni mwa Yanga lakini liliokolewa na kipa Deogratius Munishi ambaye nusura mpira umtoke na kuwa bao.

Tambwe aliyekuwa mwiba mkali kwenye safu ya ulinzi ya Majimaji, aliwanyanyua mashabiki wa Yanga kwa kufunga bao tatu kiufundi baada ya kumzidi maarifa beki wa Majimaji aliyejiangusha na kupiga shuti lililomshinda kipa aliyekuwa ametoka langoni na kutinga wavuni.

Baada ya kuzidiwa nguvu, Majimaji walifanya mabadiliko ya kuwatoa Paul Mahona na Peter Mapunda na nafasi zao kuchukuliwa na Geofrey Taita na Hassan Hamis huku Yanga wakimtoa Msuva na kumwingiza Issoufou Aboubacar.

Dakika ya 71, Tambwe alizidisha kasi ya mashambulizi na kufanikiwa kufunga bao la nne kwa kichwa akiunganisha pasi safi ya Kaseke baada ya kipa wa Majimaji kuhama langoni kwake.

Dakika ya 77 Ngoma alipata majeruhi na kushindwa kurudi uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na msahambuliaji Paul Nonga.

Yanga ilihitimisha karamu ya mabao dakika ya 83 baada ya Tambwe kufunga bao la tano kwa kutumia makosa ya kizembe yaliyofanywa na mabeki wa Majimaji na kuwafanya Wanajangwani hao kuendeleza mauaji kwa ‘Wanalizombe hao’ ambao mwaka 2005 kabla ya kushuka daraja walichapwa mabao 4-0.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, wenyeji African Sports walitoka suluhu na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga huku Mwadui FC ikiichapa Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mwadui, Shinyanga.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles