23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Mayanja atoa mkwara mzito Simba

jackson-mayanjaNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

KOCHA Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja, ametoa mkwara mzito kwa wachezaji wa timu hiyo kwa kuwataka wasikariri namba wanazocheza katika kikosi hicho kwani anaweza kufanya mabadiliko muda wowote, hivyo wanapaswa kujiweka tayari.

Kwa kuanza staili hiyo mpya ya kuwabadili namba wachezaji wake, juzi Mayanja alilazimika kumchezesha Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kama winga wa kulia badala ya beki kama anavyocheza siku zote.

Katika mchezo wa juzi uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya maafande wa JKT Ruvu, yaliyowekwa wavuni na Hamis Kiiza kwa mkwaju wa penalti na Daniel Lyanga kipindi cha pili baada ya kuingia kwa Kessy na Abdi Banda na kuiwezesha kufikisha pointi 33 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza Dar es Salaam juzi mara baada ya mchezo huo, Mayanja alisema hawezi kuangalia mchezaji amezoea kucheza namba gani ndani ya kikosi hicho ndio maana alifanya uamuzi mgumu wa kumpanga Kessy nafasi ambayo ni tofauti na alivyozoea kucheza siku zote.

“Kwenye soka hakuna kukariri namba, mchezaji anatakiwa kuwa tayari kupangwa namba yoyote uwanjani hivyo ni vyema wakafahamu jambo hili mapema kwani ninaweza kumbadili mchezaji na akacheza nafasi yoyote,” alisema.

Kocha huyo aliyeipa Simba ushindi wa pili mfululizo tangu ajiunge na kikosi hicho, aliwapongeza wachezaji Paul Kiongera, Hassan Isihaka na Kessy kwa kuonyesha kasi na uwezo vilivyosaidia kupatikana kwa ushindi.

“Wachezaji wangu wanastahili pongezi kwa kiwango walichoonyesha, sasa wanakwenda vizuri, kwa upande wa pumzi wameanza kuimarika kwani dakika 90 zimeisha hawajachoka,” alisema.

Mara nyingi Kessy akicheza kama beki wa kulia husababisha faulo nyingi zinazowapa faida wapinzani, lakini akipangwa kama winga anaweza kuisaidia timu yake na kurahisisha upatikanaji wa mabao.

Akizungumzia michuano ya Kombe la FA ambayo Simba imepangwa kucheza na timu ya Burkinafaso FC ya Morogoro, Mayanja alisema hana mpango wa kubadilisha wachezaji kwa kuwa si muda mwafaka wa kuwajaribu hivyo atachezesha kikosi kilichozoeleka ili kiweze kuongeza ushindani.

“Tunahitaji kuwa makini katika kila michuano ambayo tutashiriki kwa sasa, hakuna mpango wa kujaribu wachezaji kwa kuwadharau wapinzani wetu, kikosi kinachoshiki Ligi Kuu ndio kitaendelea kupambana kupata ushindi,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles