Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amemteua Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue Dar es Salaam jana ilieleza kuwa uteuzi huo ulianza Januari 17 mwaka huu.
Nafasi hiyo iliachwa wazi Febuari 22, 2014 baada ya kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho, Balozi Fulgence Kazaura aliyeshika wadhifa huo kwa vipindi viwili vya miaka minne.
Balozi Kazaura kwa mara ya kwanza aliteuliwa 2005 baada ya kifo cha Paul Bomani ambaye alishika wadhifa huo kuanzia 1993.
Kuteuliwa kwa Kikwete kumemfanya afuate nyayo za marais wa wastaafu waliopita; Ali Hassan Mwinyi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) na Benjamin Mkapa ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).