Theresia Gasper -Dar es salaam
TIMU ya Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 4-2, dhidi ya Friends Rangers katika mchezo wa kirafiki uliochezwa jana Uwanja wa Polisi, Kurasini, Dar es Salaam.
Yanga wanajipanga kucheza na timu ya Mbao katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Oktoba 22, mwaka huu, kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba, Mwanza.
Timu hiyo pia inakabiliwa na mchezo wa kuwania kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya Pyramid ya Misri, unaopangwa kuchezwa Oktoba 27, mwaka huu katika dimba la CCM Kirumba.
Katika mchezo wa jana, mabao ya Yanga yalifungwa na Maybin Kalengo, David Molinga na Papy Tshishimbi.
Kalengo alifunga dakika ya 23 kabla ya Molinga kufunga mawili dakika ya 24 na 27 huku Tshishimbi akitupia bao la nne dakika ya 32.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Salehe, alisema mchezo mwingine wanatarajia kuchezwa Jumatano dhidi ya Pan African kwenye uwanja huo wa Polisi.
“Baada ya mchezo huu Jumatano tutacheza mwingine ikiwa ni moja ya kuwaweka wachezaji fiti fiti kabla ya kwenda Mwanza kuivaa Mbao,” alisema. Katika hatua nyingine, Hafidhi amesema beki wao Kelvin Yondan ambaye anasumbuliwa na jeraha leo anatarajiwa kuanza mazoezi baada ya hali yake kuwa vizuri.