23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga kazi moja leo

6NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Yanga leo itakuwa na kazi moja tu ugenini kuhakikisha inavunja rekodi ya Waarabu na kuwaondosha wapinzani wao, Al Ahly ya Misri katika mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika utakaochezwa katika Uwanja wa Jeshi wa Borg Al Arab, jijini Alexandria.

Yanga imekuwa ikigonga mwamba kila inapokutana na Waarabu kwenye mechi za kimataifa, lakini safari hii kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, ametua nchini Misri akiwa na mbinu mpya ambazo anaamini zitasaidia kuwatupa nje ya michuano hiyo.

Baada ya kushtukia ujanja wa wapinzani wao wanapocheza katika ardhi ya nyumbani, Mholanzi huyo alilazimika kuwapima wachezaji wake kupitia mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar uliochezwa Jumamosi iliyopita.

Hata hivyo, kikosi cha Yanga leo kinaweza kuwa na mabadiliko makubwa tofauti na mchezo wa awali uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 9, mwaka huu kutokana na kuwepo kwa kiungo mchezeshaji, Haruna Niyonzima ambaye aliwakosa Waarabu hao katika mchezo uliopita.

Wawakilishi hao wa Tanzania, wanatakiwa kupata matokeo ya ushindi ugenini au sare ya zaidi ya mabao 2-2 ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele na kuingia hatua ya makundi, ikiwa ni baada ya kubanwa nyumbani na kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa awali.

Kabla ya mechi ya awali, benchi la ufundi la Al Ahly lilikuwa likihaha kwa muda mrefu kusaka video za mechi za Wanajangwani hao hasa ile iliyowakutanisha na APR ya Rwanda katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kujiridhisha na kiwango cha wapinzani wao.

Pamoja na jitihada hizo, bado Waarabu hao wamezidi kuihofia Yanga kutokana na kushindwa kuisoma vyema falsafa ya Pluijm, ambaye baada ya kuwashtukia alilazimika kutafuta mbinu mbadala ya kuwakabili kwa kubadili staili ya uchezaji kulingana na aina ya uchezaji wao.

Wawakilishi wengine wa Tanzania, Azam FC, jana usiku walitarajiwa kushuka dimbani kuvaana na wenyeji wao, Esperance ya Tunisia katika mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho barani Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Olympique de Rades, jijini Tunis.

Azam iliyokuwa mbele kwa ushindi wa mabao 2-1 ilioupata kwenye mchezo wa awali uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, itafanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya michuano hiyo endapo itapata matokeo ya ushindi au sare yoyote ugenini.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limezitakia kila kheri timu za Yanga na Azam katika uwakilishi wao kimataifa na kuzitaka kupambana ugenini kuhakikisha zinapata matokeo mazuri yatakayoziwezesha kuingia hatua inayofuata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles