23.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

…BMT yaipa siku 72 kufanya uchaguzi

5NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limeipa siku 72 klabu ya soka ya Yanga kuhakikisha inafanya uchaguzi wa viongozi wapya watakaoingia madarakani kwa miaka minne ijayo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya uongozi uliopo madarakani kumaliza muda wake tangu Juni mwaka 2014, ambapo inadaiwa ni kinyume na taratibu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja, alisema klabu ya Yanga inatakiwa iwe imefanya uchaguzi wake ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Alisema klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam, ilikuwa ikiendeshwa kinyume na utaratibu kutokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokuwa na sheria makini zinazoweza kutoa adhabu kwa klabu zinazoshindwa kufanya uchaguzi.

“Baraza linaiagiza TFF kuhakikisha uchaguzi wa Yanga unafanyika na mchakato unatakiwa kuanza wiki hii ili mwishoni mwa Juni mwaka huu, uongozi mpya uwe umeingia madarakani.

“Katiba itakayotumika ni ile ya mwaka 2010, viongozi watakaoingia madarakani wataingiza vipengele vya mabadiliko ndani ya katiba kama watakavyoelekezwa na TFF, kadi za wanachama zitakazotumika kwenye uchaguzi ni zile zilizotumika katika chaguzi zilizopita zenye saini ya Mwenyekiti na Katibu wa Yanga, si kadi za CRDB na Benki ya Posta,” alisema.

Kiganja alisema kwa mujibu wa maelezo ya TFF, klabu ya Yanga ilifanya Mkutano Mkuu Juni mosi mwaka 2014 ili kufanya marekebisho ya katiba ambayo hadi sasa hayajaingizwa kwenye katiba na kudai mkutano huo ndio ulimweka madarakani mwenyekiti wa sasa kwa makubaliano kwamba Oktoba 2014 uchaguzi ungefanyika.

“Sheria inaeleza kuwa uongozi wa mpito utakuwa madarakani siku 90 kabla ya uchaguzi, lakini hadi sasa uchaguzi haujafanyika na marekebisho ya katiba hayajaingizwa kwenye katiba ya Yanga kama ilivyoagizwa na TFF,” alisema Kiganja.

Aidha, baraza hilo limeiagiza TFF kuhakikisha klabu zote zinazoshiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kufanya uchaguzi mara moja isipokuwa Simba, Coastal Union na African Sports.

Pia shirikisho hilo limetakiwa kuweka sheria kali zinazotekelezeka ili kudhibiti ujanja unaofanywa na baadhi ya klabu kwa kukwepa kufanya uchaguzi.

“Ni klabu tatu tu kati ya 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ambazo zimefanya uchaguzi, pia naagiza vyama vya michezo na mashirikisho nchini kuhakikisha uchaguzi unafanyika ili kuwepo na utawala wa kisheria,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles