28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wizi TTCL unatisha

MOHAMED HABIB JUMA MNYAA-MBUNGE MKANYAGENI-CUF,BOX 2124 ZNZ.Arodia Peter na Khamis Mkotya, Dodoma

UOZO na ufisadi ulioigubika Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) uliwekwa hadharani bungeni mjini Dodoma jana. Hayo yalielezwa katika hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia.

Alisema utata katika umiliki na ukodishaji wa hisa za serikali, mikataba mibovu, madeni na baadhi ya vitu vilivyochangia kampuni hiyo kufilisika. Akisoma maoni hayo, Mohamed Habib Mnyaa alisema Serikali ilikodisha hisa 35 za TTCL kwa Kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi na kulipwa Sh bilioni 111 au asilimia 17.5.

Hata hivyo, alisema MSI hawakulipa fedha yote kwa wakati,lakini Serikali ikawapa kibali cha kuongoza Kampuni ya TTCL. “Kambi ya upinzani, inaitaka Serikali iwaeleze Watanzania ni kwa vipi hisa zinaweza kukodishwa badala ya kuuzwa na kununuliwa? Haya ni maajabu katika tasnia ya uchumi na uhasibu.

“Pia tuelezwe inakuwaje mwenye hisa asilimia 35 anakuwa na uwezo wa kuendesha kampuni wakati mwenye asilimia 65 asiwe na nafasi hiyo?” alisema Mnyaa. Mnyaa ambaye pia ni Mbunge wa Mkanyageni (CUF), alisema hivi sasa kuna mvutano mkali baina ya Serikali na Kampuni ya simu za mkononi ya Bharti Airtel kuhusu hatima ya asilimia 35 ya hisa ambazo kampuni hiyo inazimiliki ndani ya TTCL.

Akinukuu kauli ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura kwa Kamati ya Bunge, Mnyaa alisema kutokana na hasara kubwa ya Sh bilioni 334.5 mpaka kufikia mwaka 2013 na kushindwa kukopesheka huku ikibaki na mtaji wa hasi wa Sh bilioni 87.9, kwa sasa ni mufilisi.

Alisema hali hiyoimechangiwa na mbia mwenye hisa kwa asilimia 35 kutofanya uwekezaji mkubwa tangu ubia uanze mwaka 2001, jambo ambalo limesababisha uchakavu wa miundombinu na kupungua kwa ubora wa huduma.

“Kutokana na hatua hiyo, TTCL ilimtaka mwekezaji huyo kuondoa umiliki alionao ambako Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alisema kampuni hiyo ya India ambayo ni kampuni mama ya Airtel Tanzania, inataka ilipwe Sh bilioni 14 ingawa haijawahi kuwekeza chochote ndani ya TTCL kama ilivyo kwa watangulizi wake, yaani Celtel Tanzania, Celtel International na Zain.

“Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Patrick Makungu alisema Baraza la Mawaziri limeunda jopo la majadiliano na mwekezaji huyo kuzungumzia gharama za kumlipa aweze kuondoka TTCL na kwamba hakuna taarifa kuhusu fedha zilizotajwa. Alisema hata njia za simu 800,100 walizoahidi hawakuzijenga badala yake zile walizozikuta 270,000 walizipunguza na kufikia 158,000 tu. Alisema Airtel ilianzishwa kwa fedha, leseni na raslimali za TTCL mpaka sasa inatumia miundombinu ya TTCL ikiwamo jenereta, majengo, viwanja.

Katika kashifa hiyo, Mnyaa pia alifichua taarifa kwamba kati ya wakurugenzi wawili waliosaini mkataba wa kukodisha hisa hizo asilimia 35 za TTCL kwa MSI, wakati huo ni aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na baadaye akateuliwa kuwa mkuu wa wilaya. Mfumo wa uendeshaji wa Kampuni ya TTCL ni mbaya usiojali maslahi ya nchi, wafanyakazi na wateja, alisema. Alisema kuna meneja alikutwa kwenye akaunti yake akiwa na Sh bilioni moja.

“Kuna wizi ambao umeota mizizi katika shirika hili,wakuu wa idara wanajilipa mafao yao ya kustaafu, lakini wanajigeuza na kujiongezea mikataba ya ajira, tena kibaya zaidi wanaendelea kushikilia nyadhifa zile zile,”alisema Mnyaa. Kutokana na sababu hizo Juni 12, 2012, watumishi wa TTCL walimwandikia barua waziri mkuu kueleza madhira yanayofanywa na menejimenti ya TTCL kabla ya kamati ya wafanyakazi kuandika barua kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akafanye ukaguzi maalum lakini hadi sasa hakuna hatua zilizokwisha kuchukuliwa.

Wabunge wazituhumu kampuni za simu kuwaibia wananchi Vifurushi vya simu Baadhi ya wabunge wamezituhumu kampuni mbalimbali za simu nchini kuwa zimekuwa zikiwaibia wananchi kupitia huduma zao za vifurushi (bundle). Wakizungumza bungeni, wabunge hao walisema wananchi wamekuwa wakikatwa fedha zao katika simu kwa huduma ambazo hawakuziomba, jambo ambalo walisema ni wizi.

Katika mchango wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Midimu (CCM), alishangazwa na utaratibu wa makampuni ya simu za mikoni kubadilisha gharama za vifurushi. “Ni mwaka jana tu ilikua ukinunua bundle (kifurushi) la Sh 2,800 unapata dakika 105, lakini hivi sasa ukinunua kifurushi cha gharama hiyo hiyo unapata dakika 85.

“Hivi ina maana kila mwaka system (mfumo) inabadilika? Watu wanakatwa fedhaholela kwenye simu, wanakatwa Sh 400 kila mwezi, wanakuletea ujumbe mfupi wimbo wako umewekwa upya,” alisema.

Naye Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), alisema makampuni hayo yamekuwa yakiwanyonya wananchi kwa kuwakata fedha nyingi ambazo hazilingani na huduma.
Profesa Mbarawa Waziri wa Mwasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa katika bajeti yake alisema Serikali imeingia makubaliano ya ushirikiano na Kamapuni mpya ya Viettel ya Vietnam kwa lengo la kuweka mawasiliano.

Katika ushirikiano huo, kampuni hiyo itajenga miundombinu ya mkongo wenye urefu wa kilometa 13,000 kwa kutumia nguzo za miti katika wilaya zote nchini katika mwaka mmoja na itakamilika Julai 2016. Mbarawa aliliomba Bunge liidhinishe Sh bilioni 66,939,615, kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2015/16.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles