24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Al Shabaab waua polisi 25 Kenya

Uhuru_M_Kenyatta_685841119NAIROBI, KENYA
KUNDI la wana mgambo wa Al Shabaab la Somalia, linadaiwa kuwaua polisi 25 wa Kenya jana.
Inaelezwa kuwa wanamgambo hao walivamia magari ya polisi katika eneo la Yumbis wilayani Fafi, Kaunti ya Garissa.
Hadi jana jioni, hakukuwa na taarifa inayoeleza waliko polisi walionusurika baada ya shambulio hilo la kushtukiza.
Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Daily Nation, zilisema maofisa watatu walionusurika shambulio hilo walisema magari manne ya polisi yaliteketezwa na wanamgambo hao.
Maofisa hao walikuwa kwenye msafara huowakielekea Yumbis saa chache tu baada ya wenzao wengine kujeruhiwa kwenye shambulio la Jumatatu alasiri.
Katika shambulio la kwanza, maofisa watatu walijeruhiwa baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa na wanamgambo hao.
Mwakilishi wa Kata ya Jarajila, Mahat Osman alisema maofisa hao walikuwa wakienda Yumbis wakati gari lao lilipokanyaga bomu katika eneo la Yarey.
Alisema waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Garissa.
Mkuu wa Wilaya ya Fafi, Geoffrey Taragon alisema hali za askari hao ni mbaya.
Mashambulio dhidi ya askari hao wa Kenya yalitokea ikiwa ni wiki moja tu baada ya Al- Shabaab kuvamia Kijiji cha Yumbis na vingine jirani na kuwahutubia wakazi wake msikitini kwa saa kadha bila mamlaka za usalama za Kenya kujua kilichokuwa kinaendelea.
Kundi hilo lenye uhusiano na mtandao wa ugaidi wa al Qaeda, lilisema liliwashambulia polisi kilomita 70 kaskazini mwa Garissa, mji ambao wanamgambo hao walivamia Chuo Kikuu cha Garisa na kuua watu 148 wengi wao wakiwa wanafunzi, Aprili mwaka huu.
Wanamgambo hao wanaopigania kuiangusha Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na nchi za magharibi, wameanzisha mashambulio mengi ndani ya ardhi ya Kenya wakijaribu kuilazimisha iondoe askari wake Somalia.
Mashambulio hayo yamesababisha Serikali ya Kenya izidi kubanwa iondoe askari wake Somalia lakini imeapa kuendelea na operesheni yake sambamba na majeshi mengine ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika (AU) nchini humo.
Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imeendelea na msimamo huo licha ya watu kuendelea kuuawa nchini Kenya kwa mashambulio ya wanamgambo hao huku sekta ya utalii, ambayo ni miongoni mwa vyanzo vyake vikuu vya fedha za kigeni ikiporomoka.
Katika tukio la jana, Jeshi la Polisi lilisema ni askari mmoja tu aliyeuawa katika mashambulio hayo ya Fafi na Yumbis na mwingine alijeruhiwa vibaya, huku watatu wakiwa na majeraha madogo.
“Kundi la maofisa lililopelekwa kuongeza nguvu wakati lilipowasili eneo la tukio lilijikuta likishambuliwa kwa kushtukizwa,” Mkuu wa Jeshi la Polisi, Joseph Boinnet alisema katika taarifa yake jana.
Lakini wakati taarifa za awali za vyombo vya habari zikisema askari zaidi ya 20 hawajulikani waliko, kundi la al Shabaab lilisisitiza kuua askari 25.
“Tumechukua silaha zao zote. Kulikuwa na askari wa Kenya waliokuwa wakikimbia huko na huko baada ya shambulio hili la kushtukiza,” msemaji wa operesheni za kijeshi wa al Shabaab, Sheikh Abdiasis Abu Musab, alisema.
Majeshi ya AU na Somalia, yamefanikiwa kuwaondoa Al Shabaab kutoka miji mikubwa ya Somalia katika miezi ya hivi karibuni.
Lakini shambulio la jana, linazidi kudhihirisha kwamba kundi hilo bado lina uwezo mkubwa wa kufanya mashambulio katika maeneo muhimu ya Kenya.
Sababu za mashambulio
Jeshi la Kenya liliingia kusini mwa Somalia, Oktoba 2011 baada ya mlolongo wa matukio ya utekaji nyara watalii na wafanyakazi wa kigeni wa mashirika ya misaada ndani ya ardhi ya Kenya, yaliyofanywa na kundi hilo ambalo hata hivyo lilikana kuyaendesha.
Tangu kipindi hicho yamekawapo mashambulio ya mara kwa mara, mengi yakiwalenga raia.

Watu 400 wameuawa
Al Shabaab limekwisha kuwaua watu zaidi ya 400 nchini Kenya tangu Rais Uhuru Kenyatta aingie madarakani Aprili, 2013.
Mashambulio yameendelea bila kukoma licha ya utawala huo kujaribu kuzuia uingizaji wa silaha kwa magendo katika mpaka wake na Somalia wenye urefu wa kilomita 700.
Shambulio kwenye Chuo Kikuu cha Garissa mwezi uliopita ndilo lililoua watu wengi kwa wakati mmoja kuliko lile la Westgate mjini Nairobi, Septemba 21, 2013 ambako watu 67 waliuawa.
Baada ya shambulio la Westgate, Wakenya walidhani ulinzi umeimarishwa, lakini Desemba 13, 2013, mashambulio pacha katika mji wa kaskazini mashariki wa Wajir yaliua watu wawili na kujeruhi wengine watatu.
Siku iliyofuata kundi hilo, lilirusha bomu la kutupa kwa mkono katika basi dogo katika kitongoji cha Eastleigh, Nairobi na kuua watu wanne na kujeruhi wengine 36.
Hilo lilikuwa shambulio la nne kutokea wakati wa wiki ambayo Kenya ilikuwa ikiadhimisha miaka 50 ya uhuru wake.
Machi 31, 2014, mabomu mawili yaliua watu sita katika eneo linalokaliwa na Wasomali wengi la Eastleigh jijini Nairobi.

Aprili Mosi, 2014 katika eneo hilo hilo, watu sita walikufa na wengine wengi kujeruhiwa wakati mabomu yalipolipuka katika maeneo mawili tofauti yakiwa yameachana umbali wa mita 300.
Kati ya Aprili 9, 2014 na Mei 23, 2014 yalikuwapo mashambulio mengi yakienda sambamba na kukamatwa kwa magaidi au silaha katika maeneo mbalimbali ya Nairobi na Mombasa, ambako watu 13 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Watalii wakimbia
Hali kadhalika Juni 16, 2014, Al-Shabaab waliua watu 48 walipovamia mji wa pwani wa Mpeketoni kwa kushamulia kituo cha polisi, hoteli na ofisi za Serikali na kusababisha watalii kupungua kwa kiasi kikubwa.
Mwishoni mwa mwaka 2014, mashambuilio mawili ya Al Shabaab yaliua watu 64 katika Kaunti ya Mandera.
Katika shambulio la kwanza, wanamgambo walishambulia basi lililokuwa likisafiri kutoka Mandera kwenda Nairobi na kuua watu 28.
Mwezi huo huo, Al-Shabaab walishambulia wafanyakazi waliokuwa machimboni na kuua 36, wengi wao wakiwa si Waislamu, karibu na mji huo wa Mandera.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles