30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

WIZARA YA VIWANDA YAJA NA VIPAUMBELE 13

GABRIEL MUSHI NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA


WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/19 na kuliomba kuidhinishiwa Sh bilioni 143.3, huku akibainisha vipaumbele 13 kwa mwaka wa fedha ujao.

Akiwasilisha hotuba yake bungeni jijini Dodoma jana, Mwijage alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 43.3 ni za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 100 ni za maendeleo.

Alisema bajeti ya mwaka huu ni ongezeko la asilimia 17.28 ikilinganishwa na ya mwaka 2017/18 ambayo ilikuwa Sh bilioni 122.2.

Vipaumbele 13

Mwijage alisema vipaumbele vya wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi zake ni kutunisha mtaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF); kuendeleza miradi ya kielelezo ya Mchuchuma na Liganga kwa kulipia fidia, mradi wa magadi Soda Engaruka na Kiwanda cha Matairi Arusha.

Pia kuendelezaji wa eneo la Viwanda TAMCO Kibaha, mradi wa kuunganisha matrekta ya URSUS, uendelezaji wa Mitaa/maeneo ya viwanda vya SIDO,  kuendeleza Kanda Kuu za Uchumi (Ruvuma, Tanga, Kigoma na Manyoni).

“Pia kuendeleza mradi wa Bagamoyo SEZ & BMSEZ, kurasini Logistic Centre and Kigamboni Industrial Park, kuendeleza utafiti kwa ajili ya TIRDO, CAMARTEC na TEMDO, Dodoma Leather and Dodoma SEZ na ujenzi wa maeneo maalumu ya viwanda,” alisema.

Alisema pamoja na vipaumbele hivyo, wizara itaweka msukumo wa pekee katika kuhamasisha ujenzi wa sekta binafsi ya Kitanzania iliyo imara ili iweze kushiriki na kuchangia ipasavyo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Viwanda vipya 3,306

Alisema kutokana na umuhimu wa sekta ya viwanda, tangu Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani viwanda vipya 3,306 vimejengwa mpaka kufikia Machi  mwaka huu.

“Awali Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda 53,876,kati ya viwanda vikubwa ni 251, vya kati ni 173, vidogo ni 6,957 na vidogo sana ni 46,495,” alisema.

Ufufuaji wa viwanda

Aidha, alisema hadi kufikia Mei mwaka 2017, viwanda 62 vilikuwa vinafanya kazi vizuri, 28 vilikuwa vinafanya kazi chini ya kiwango, 56 vilikuwa havifanyi kazi kabisa na 10 vilikuwa vimeuzwa kwa mali moja moja.

“Kuanzia Agosti 2017 hadi Machi 2018, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina na wizara za kisekta ilifanya tena tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa, ili kubaini hali ya viwanda hivyo baada ya kufanya zoezi la kuhamasisha ufufuaji wake.

Aidha, alisema kuanzia Julai 2017 mpaka Machi mwaka huu, jumla ya miradi mipya 243 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 4,169.11 inayotarajiwa kuajiri watu 44,798 ilikuwa imesajiliwa.

Viwanda vidogo

Mwijage pia alizungumzia maendeleo ya viwanda vidogo na kubainisha kuwa sekta hiyo ni muhimu katika ustawi wa Taifa kwa kuwa inachochea ujenzi wa uchumi jumuishi.

Alisema sekta hiyo kwa sasa inaajiri watanzania milioni sita na viwanda hivyo vinachangia Pato la Taifa kwa takriban asilimia 35.

“Viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati vimechukua zaidi ya asilimia 98 ya idadi ya viwanda nchini na wawekezaji wa viwanda katika kundi hilo ni watanzania wenyewe,” alisema na kuongeza:

“Wizara imeandaa na kukamilisha mwongozo wa kusimamia maendeleo na ujenzi wa viwanda nchini, utakaowezesha mikoa na wilaya kusimama ujenzi wa viwanda kwa ufanisi na tija.”

Malengo ya sekta ya viwanda

Pamoja na mambo mengine alisema katika mwaka 2018/2019, sekta ya viwanda ina malengo kufanya tathmini ya hali halisi ya uzalishaji viwandani na mahitaji ya bidhaa za viwanda  katika sekta ya sukari, mafuta ya kula, vifaa vya ujenzi na chuma.

Aidha, alisema Tume ya Ushindani (FCC) ilifanya ukaguzi katika bandari ya Dar es Salaam na nchi kavu ambako jumla ya makontena 4,004 yalikaguliwa na kati ya hayo, makasha 415 yalibainika kuwa na bidhaa mbalimbalin zilizokiuka sheria ya alama za bidhaa ya mwaka 1963.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles