32.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI 40,000 ELIMU YA JUU KUPEWA MIKOPO

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


ZAIDI ya wanafunzi 40,000 wa mwaka wa kwanza wa vyuo vya elimu ya juu, wanatarajia kupata mikopo katika mwaka wa masomo wa 2018/2019.

Dirisha la maombi ya mikopo lilifunguliwa jana na linatarajiwa kufungwa Julai 15 mwaka huu huku bajeti ya fedha za mikopo kwa mwaka 2018/2019 ikiwa ni Sh bilioni 427.

Hata hivyo wakati dirisha hilo likifunguliwa, bodi hiyo imesisitiza   waombaji ambao wazazi/walezi ni wamiliki wa biashara, mameneja wakubwa katika mamlaka zinazotambulika, hawaruhusiwi kuomba mkopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru, alisema jana kuwa kati ya wanafunzi hao, 14,000 ni wanawake na 26,000 ni wanaume.

Alisema wanafunzi 80,000 wanaoendelea na masomo nao watapatiwa mikopo.

“Mikopo si zawadi hivyo unapoamua kuomba ni lazima ukumbuke kwamba utalipa. Wadhamini wahakikishe mwombaji analipa mkopo husika vinginevyo watawajibika kisheria kulipa,” alisema Badru.

Alisema kipaumbele kitatolewa kwa wanaotaka kusoma kozi zenye mahitaji zaidi kama vile walimu wa masomo ya sayansi na hisabati, sayansi ya afya ya binadamu, uhandisi wa aina zote, sayansi za kilimo na wanyama na masuala ya gesi na nishati.

Alisema pia kwa waombaji ambao ni yatima na wenye nakala za vyeti vyua vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) nao watapewa kipaumbele bila kujali kozi wanazosoma.

“Wengine watakaopewa kipaumbele ni waombaji wenye ulemavu uliothibitishwa na mganga mkuu wa mkoa au wilaya na waombaji ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya stashahada au sekondari wawe na barua za uthibitisho kutoka taasisi zilizowafadhili,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema wametanua wigo wa kutoa mikopo kwa baadhi ya wanafunzi wa stashahad na kuwaomba wazazi wenye uwezo kuwasomesha watoto wao ili mikopo isaidie watoto wanaotoka katika familia zisizoweza kujilipia.

Bodi hiyo ilisema pia kuwa mwaka huu maofisa wa bodi watatembelea mikoa mbalimbali  kukutana na waombaji   kuwaelimisha kuhusu taratibu za kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandao.

VIGEZO

Bodi hiyo imetoa mwongozo wa uombaji mikopo na kitabu chenye maswali 21 kuhusu sifa na utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mikopo.

Mbali na sifa za jumla, vigezo vya ziada vimesisitiza mwanafunzi mhitaji asizidi miaka 33 katika kipindi anachoomba mkopo.

Waombaji ambao wazazi/walezi ni wamiliki wa biashara, mameneja wakubwa katika mamlaka zinazotambulika zenye usajili hawaruhusiwi kuomba mkopo.

Lazima awe amedahiliwa kutoka taasisi ya elimu ya juu kwa muda wote isipokuwa wanafunzi waliodahiliwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Malipo ya ada iliyolipwa sekondari na diploma ni kigezo kimojawapo kinachoangaliwa kuwa na uwezo wa kuchangia gharama za elimu ya juu. Vingine ni uyatima, ulemavu, udhamini na familia maskini.

RITA

Naye Meneja Usajili kutoka RITA, Patricia Mkuya, alisema wanatarajia kuhakiki vyeti vya wanafunzi 60,000 waliozaliwa Tanzania Bara katika mwaka wa masomo wa 2018/2019 wakati kwa wanafunzi waliozaliwa Zanzibar vyeti vyao vitahakikiwa huko huko.

Alisema wanafunzi wanaweza kwenda kuhakikiwa katika ofisi za wakuu wa wilaya walikopata cheti za kuzaliwa au kutumia mfumo wa mtandao wa intaneti hasa kwa wale wanaoishi mbali na wilaya husika na   Dar es Salaam.

“Tunasisitiza matumizi ya mtandao   kupunguza mrundikano katika ofisi za wakala na kuwapunguzia usumbufu waombaji.

“Mwanafunzi anaweza kutuma nyaraka zake na kuendelea na masomo bila kuja ofisi za RITA na atajibiwa ndani ya siku tatu,” alisema Mkuya.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (TAHLISO), George Mnali, aliiomba bodi hiyo kuwafikiria wanafunzi waliokosa mikopo mwaka jana kwa sababu wengi wana hali ngumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles