Na Mwandishi wetu   |
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa ufafanuzi kuhusu vitabu vyenye makosa vinavyosambaa mitandaoni vikionyesha picha inayoelezea viungo vya mwili wa binadamu.
Kitabu hicho kilisambaa mitandaoni jana, na moja ya kurasa zake inaonyesha sehemu mbalimbali kwa njia tofauti ambapo shingo inaonyesha kifua, paja (kiuno), kichwa (nyusi), sikio (shingo) na sehemu nyingine mbalimbali za mwili.
Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mwasu Sware, kitabu kinachosambazwa si chapisho la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), na wala si miongoni mwa vitabu ambavyo vimesambazwa kwenye shule.
“Pia kitabu kinachosambazwa hakina uhusiano wowote na wala hakifanani na vitabu ambavyo vimechapishwa hivi karibuni na TET.
“Wizara inawasihi Watanzania kupuuza taarifa hizo zenye nia ya kupotosha,” imesema taarifa hiyo ya Mwasu.