24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

GHOROFA LA JOTI KUBOMOLEWA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


GHOROFA la Muigizaji, Lucas Mhuvile maarufu kama Joti, lililoko katika eneo la Kibada Wilaya ya Kigamboni, limewekwa alama ya X na kutakiwa kubomolewa.

Nyumba ya Joti na nyingine zilizoko pembeni ya barabara ya Kibada zinatakiwa kubomolewa kupisha upanuzi wa barabara hiyo.

Alama hizo za X zilizowekwa na Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam zimezua taharuki kubwa baada ya baadhi ya wananchi kudai kuwa walijenga kwa halali na hawakuifuata barabara.

Hali hiyo iliilazimu Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kigamboni ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hashim Mgandilwa, kutembelea eneo hilo kujionea hali halisi na kuzungumza na wananchi.

Joti alikuwa miongoni mwa wananchi waliojitokeza jana na wakati kamati hiyo ikikagua mawe ya alama alionekana akisaidiana na wenzake kuyaonyesha.

Mgandilwa alichimba sehemu ya kwanza ambako ilidaiwa kuwa jiwe lilikuwa limefukiwa lakini halikuonekana na kuamua kwenda sehemu nyingine.

“Mheshimiwa DC twendeni pale kwangu nikawaonyeshe jiwe liliko,” alisema Joti huku akiongozana na kamati hiyo.

Kamati hiyo ilipofika katika eneo la Joti iliangalia jiwe kisha kwenda jirani na eneo hilo kuangalia mawe mengine.

Licha ya kuonyesha mawe Joti na wenzake walionekana wakiangalia ramani ya eneo hilo na kumuonyesha Mgandilwa mahali yaliko maeneo yao.

Kuna wakati Mkuu huyo wa wilaya alilazimika kutumia futi kupima urefu wa kuanzia yalipo mawe hadi zilipowekwa alama za X.

Mkazi mwingine wa Kibada, Mwanahamisi Abdallah, alisema wameshangazwa na hatua hiyo kwa sababu waliuziwa maeneo hayo kwa halali na serikali.

“Kulikuwa na mradi wa upimaji na uuzwaji viwanja katika eneo hili na sisi tuliuziwa kwa halali na kupewa hati.

“Lakini tumeshangaa wiki mbili zilizopita tuliona watu wanapita kwenye makazi yetu na  kuweka alama za X kwamba tubomoe,” alisema Abdallah.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Assah Simba, alisema uwekaji alama hizo umesababisha baadhi ya wakazi kushindwa kufanya biashara kwa kuhofia kubomolewa wakati wowote.

“Baadhi yetu tuna maduka ya biashara lakini tunashindwa kuyapangisha kwa sababu mtu anakuja anakuta kuna alama ya X anahofia kufanya biashara.

“Ili kutenda haki tunaomba alama za X ziondolewe vinginevyo tutaanzisha migogoro mingine,” alisema Simba.

Baada ya kusikiliza hoja za wananchi hao Mgandilwa aliwataka wote waliowekewa X wafike ofisini kwake Jumamosi wakiwa na nyaraka halali za maeneo husika.

“Kuna watu walikuja ofisini kulalamika ndiyo maana tumekuja tujionee hali halisi kwa sababu hakuna serikali inayotaka kumwonea mtu. Tunatakiwa tutengeneze usawa.

“Kama una ofa, hati au kibali cha ujenzi njoo navyo na uonyeshe eneo lililokatwa na barabara,” alisema Mgandilwa.

Kwa mujibu wa Mgandilwa, alama hizo zimewekwa kuanzia eneo la Kimbiji, Pembamnazi, Kisarawe 11 na Kibada.

Alisema baada ya kukagua mawe ya alama yaliyowekwa na TANROADS, Wizara ya Ardhi na mahali zilipowekwa alama X alibaini ni maeneo matatu tofauti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles