25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

WHO, UNFPA WATOA MSAADA WA MAGARI 58

 Waziri Ummy Mwalimu
Waziri Ummy Mwalimu

NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA), wameipa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto magari 58.

Who imetoa msaada wa magari 50 ya kubebea wagonjwa (Ambulance) na UNFPA imetoa magari manane ambayo yatatumika kuratibu shughuli za afya ya mama na mtoto.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya makabidhiano ya magari hayo,  Waziri Ummy Mwalimu, alisema yatagawiwa katika mikoa sita iliyopo Kanda ya Ziwa.

“Tafiti zilizofanywa mwaka 2010 na tathmini iliyofanywa mwaka 2015 wakati wa kuandaa Mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BRN), mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwamo Kigoma ilionekana kuwa na viashiria hafifu vya afya ya mama na mtoto,” alisema.

Akitolea mfano alisema mikoa hiyo ilionekana kuwa na utumiaji mdogo wa huduma ya uzazi wa mpango, wanawake wachache ndio waliojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuna idadi kubwa ya vifo.

“Wanawake wengi wanafariki dunia kwa uzazi nchini, hii ni changamoto kubwa kwetu, tumepambana kwa miaka 20 tumefanikiwa kuvipunguza kutoka vifo 580 hadi 432 kwa kila vizazi hai 100,000.

“Nia yetu ifikapo 2020 tuweze kupunguza tena idadi hiyo kutoka 432 hadi 292 sawa na asilimia 30 pamoja na vifo vya watoto wachanga kuvipunguza kutoka 54 ya sasa hadi 40 kwa kila vizazi hai 1,000,” alisema na kuongeza:

“Hivyo magari haya yatapelekwa katika mkoa wa Mwanza, Geita, Kigoma, Simiyu, Kagera na Mara.

Aliwataka waganga wakuu wa mikoa ambao watakabidhiwa magari hayo kuyakatia bima ya ajali ili yaendelee kudumu kutoa huduma kwa wananchi.

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA-Tanzania, Dk. Hashina Begum, alisema magari hayo manane waliyoyatoa yana thamani ya Sh milioni 387.

“Tuna imani kwamba yatakuwa msaada mkubwa kwa Serikali katika kusimamia shughuli zote za uratibu wa afya ya mama na mtoto na hivyo kufikia lengo la kupunguza idadi ya vifo iliyotajwa,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa WHO, Dk. Grace Saguti, alisema ambulance hizo zilizotolewa zitakuwa na huduma zote muhimu.

“Tumetanguliza hizi 50 zenye thamani ya Sh bilioni 5.9, lengo letu ni kuipatia wizara ya afya jumla ya ambulance 67,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles