Shirika la Afya Duniani WHO limesema zaidi ya watu 30,000 wamepoteza makazi yao kutokana na vita vinavyoendelea karibu na mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeandika jana katika ukurasa wake wa Twitter kwamba watu wapatao 227 wameuawa na zaidi ya 1,125 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.
Mapigano hayo nchini Libya yalianza tangu Aprili 4 baada ya mbabe wa kivita Khalifa Haftar kuliamrisha jeshi lake la Libya National Army (LNA) kuipokonya udhibiti wa mji mkuu -Tripoli serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Tangu wakati huo mapigano yanayohofiwa kuchochea zaidi mgogoro wa Libya yamekuwa yakiendelea kati ya pande hizo mbili nje ya Tripoli.