Na RENATHA KIPAKA
-Bukoba
WATU wenye ualbino Manispaa ya Bukoba, wameiomba Serikali wilayani humo kuwasaidia kuimarisha ulinzi na katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Walisema wakati wa uchaguzi, hulazimika kusimamisha shughuli za uzalishaji na kukaaa ndani kwa hofu ya usalama wa maisha yao.
Agusta Agustine, mkazi wa Kata ya Nshambya aliiambia Mtanzania kuwa huingiwa na hofu ya kupoteza maisha kutokana na kuripotiwa kwa matukio ya ukatili kwa watu wenye ulemevu huo.
“Maisha ya hofu yanaingia unaposikia sehemu nyingine ndani ya wilaya au nje ya mkoa mtu kama mimi amefanyiwa ukatili, kutolewa viungo kwenye mwili au kufa …jamani tupendane,” alisema Agustine.
Frolence Frolian mkazi wa Mtaa wa Buyekera Kata Bakoba alisema wameamua kuomba msaada kwa Serikali kabla harakati za viongozi wanaogombewa nafasi hawajaanza kufanya kampeni.
“Endapo viongozi wetu wa dini na wadau wakiingilia kati kutoa elimu kwa wanasiasa na waganga wa jadi, unyanyasaji na ukatili vitaondoka hasa maeneo kama Ngara na nje ya mkoa kama Shinyanga,” alisema Frolian.
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mkoa wa Kagera, Nsubisi Mwakisambwe, alisema ushirikishwaji wa jamii kwenye masuala ya matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani ni njia moja wapo ya kutatua changamoto.
Mwakisambwe alisema njia hiyo ni msaada pekee wa kujua usalama kwa kila hatua inapooneka kuna hali yoyote katika mazingira ya wanajamii hasa.
Alisema mikakati iliyopo ni kutambua idadi kamili ya watu hao na kuwapatia viongozi wa mitaa ambao watakuwa washirIki zaidi katika ulinzi na usalama kwa kuitisha mikutano shirikishi ya kuwapa elimu wana jamii.
Naibu Meya wa Halmashauiri ya Manispaa ya Bukoba, Jimmy Kalugendo, alisema wanasiasa ndiyo wamekuwa walengwa wa kudhaniwa ni watatafutaji kura kwa njia zisizokuwa sahihi na hushirikiana na waganga wa jadi.
Alisema watambue kuwa upatikanaji wa kura siyo kwa kukatili maisha ya mwanadamu bali watumie kauri zao zenye kushawishi wananchi kutoa kura kwa nia njema na ya amani na siyo kuondoa uhai wa mtu.
“Nafasi ya uongozi inakuja kwa kujinadi kwa wapiga kura na kuwatekelezea yale ambayo yanatakiwa na sio vitendo vya ukatili vinavyotoolewa taarifa nyakati za uchaguzi.
“Nafasi nzuri ni matekelezo ya wananchi,” alisema Kalugendo.