27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Bageni akata rufaa kupinga kunyongwa

NA KULWA MZEE

DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA  Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni,   Christopher Bageni, aliyehukumiwa kunyongwa   kwa kuua wafanyabiashara wa madini, amepinga adhabu hiyo na maombi yake yanatarajiwa kusikikizwa Juni 16.

  Bageni amewasilisha maombi ya mapitio Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambayo yamepangwa kusikikizwa mbele ya jopo la majaji watatu, Stellah Mugasha, Fednand Wambali na Rehema Kerefu.

Katika maombi ya mapitio aliwasilisha sababu mbalimbali za kupinga adhabu hiyo ikiwamo kwamba jopo la majaji lilifanya makosa ya dhahiri katika muonekano na hivyo kusababisha haki kutozingatiwa.

 Bageni alihukumiwa adhabu hiyo Septemba 16 mwaka 2016 na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania mbele ya jopo la majaji watatu, Jaji Benard Luanda, Sauda Mjasiri na Senistocles Kaijage.

Mahakama ya Rufaa ilitoa hukumu hiyo baada ya kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP) akipinga aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO),   Abdallah Zombe na maofisa wenzake watatu akiwamo Bageni kuachiwa huru na Mahakama Kuu mwaka 2009.

Hukumu hiyo ilisomwa na aliyekuwa Msajili wa Mahakama ya Rufaa wakati huo, Jaji  John Kahyoza.

Aliwataja wajibu rufani kuwa ni Zombe,   Bageni, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Urafiki,   Ahmed Makelle na Rajabu Bakari.

Alisema Mahakama ya rufaa ilipitia ushahidi uliotolewa Mahakama Kuu na kuona mahakama hiyo ilishindwa kuwatia hatiani washtakiwa kwa mauaji na kwa kosa la kusaidia mauaji kufanyika.

“Kosa la kuua na kosa la kusaidia kuua ni makosa mawili tofauti, si sahihi kwa mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji kutiwa hatiani kwa kosa jingine ambalo tangu mwanzo mshtakiwa alitakiwa kulijua  aweze kujitetea.

“Makosa hayo si makosa yanayofanana hivyo mahakama hiyo ilitofautiana na hoja za upande wa Jamhuri kwamba washtakiwa watiwe hatiani kwa kosa la kusaidia kuua baada ya kushindwa kutiwa hatiani kwa mauaji.

“Washtakiwa wote katika utetezi wao walipinga kuhusika katika mauaji hayo lakini mjibu rufani wa nne, Rajabu alisema ukweli katika ushahidi wake kwa kueleza tukio la mauaji lilivyofanyika katika Msitu wa Pande.

“Pamoja na mjibu rufani kusema ukweli lakini ushahidi wake ulitakiwa kupokelewa kwa makini na unatakiwa kuwapo   ushahidi mwingine wa kuunga mkono.

“Mjibu rufani wa kwanza mahakama haioni kama kuna ushahidi wa kumtia hatiani kwa mauaji wala kwa kusaidia kuua japo kuna jambo kichwani mwake analolifahamu kuhusu mauaji hayo.

“Ushahidi mwingine unaonyesha wajibu rufani watatu walishuhudia mauaji lakini hawakuua,” lilisema jopo.

Jopo lilisema wamekubaliana kwamba watu wanne waliuawa kwa bunduki na mauaji yalikuwa ya kinyama katika Msitu wa Pande.

Mahakama hiyo ilijiuliza maswali kwamba je, wajibu rufani walikuwapo Pande, jibu ni kwamba wajibu rufani 2,3,4 walikuwapo katika msitu huo na mjibu rufani wanne alisema ukweli mahakamani kuhusiana na tukio hilo.

Ilidaiwa kwamba mauaji hayo yalifanywa na polisi, Sadi lakini mshtakiwa huyo hajawahi kushtakiwa lakini mahakama inajiuliza marehemu walipelekwa Pande kwa amri ya nani.

“Mahakama inajiuliza nini nia ya kuwapeleka marehemu Pande sehemu ambayo haina hata nyumba, mjibu rufani wa pili, Bageni ndiye alitoa amri ya kuua, ushahidi unaonyesha marehemu walipelekwa Pande na washtakiwa walikwenda Pande.

“Marehemu walipelekwa huko ili tukio la mauaji lifanyike bila kipingamizi kwa kibali cha Bageni, ushahidi wa mjibu rufani wanne uliungwa mkono na tabia ya Bageni kwamba alikuwa akificha ukweli kuhusu mauaji hayo.

“Kulikuwa na ushahidi wa maofisa watatu wa polisi, wote walidanganya kwamba mauaji yalitokea Sinza katika majibizano kati ya polisi na marehemu wakati wengine wa Sinza walisema hawakusikia tukio la aina hiyo kutokea.

“Mjibu rufani wa 1,3,4 rufani dhidi yao inatupwa hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani, mjibu rufani wa pili mahakama inatengua kuachiwa kwake kutiwa hatiani na Mahakama Kuu, inamuhukumu kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya watu wanne,”alimalizia kusoma hukumu hiyo.

Wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Morogoro waliouawa ni Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi, mkazi wa Manzese Dar es Salaam, Juma Ndugu.

Walidaiwa kutenda makosa hayo Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande  wilayani Kinondoni baada ya kuwakamata wafanyabiashara hao Sinza, walipokuwa Dar es Salaam kuuza madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles