23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

KAGERA SUGAR YAPETA

Na WINFRIDA MTOI

-DAR ES SALAAM

BODI ya Ligi Tanzania (TPLB) imekiri kufanya makosa katika uwekaji takwimu na kuitangaza Kagera Sugar kuwa timu iliyoshuka daraja moja kwa moja badala ya Stand United.

Kagera Sugar ilicheza mechi yake ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya  Mbao FC na kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Sare hiyo iliifanya ifikishe pointi 44, sawa na Stand United iliyofungwa mabao 2-0 na JKT Tanzania.

Baada ya matokeo hayo, Kampuni ya Azam Media kupitia runinga yake ya Azam yenye   dhamana ya kurusha michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ilianika msimamo  ukionyesha Stand United imeshuka daraja, lakini ule wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ulionyesha Kagera Sugar  ndiyo imeaga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura, alisema  takwimu za awali zilionyesha  Kagera Sugar imemaliza ikiwa nafasi ya 19 na Stand United 18 kutokana na utofauti wa mabao ya kufungwa na kufunga.

Alisema baada ya kufanyiwa marekebisho kwa kupitia  tena takwimu, walibaini timu inayostahili kuungana na African Lyon kushuka daraja ni Stand United huku  Kagera Sugar ikitakiwa kucheza hatua ya  mtoano ‘Play Off’ pamoja na Mwadui FC.

Wambura alifafanua kuwa, licha ya timu hizo kulingana pointi  ambazo ni 44, Kagera Sugar ina faida ya tofauti kubwa ya  mabao ya kufunga na kufungwa ambayo ni  hasi 10 wakati Stand United ina hasi 12.

“Katika msimamo wa kwanza hadi kufikia hatua ya kuitangaza Kagera kuwa imeshuka, tuliangalia kanuni, timu zinaanza kutenganishwa kwa pointi, zikilingana zinatenganishwa kwa tofauti ya mabao, zikilingana tunakwenda kwa timu iliyofunga mabao mengi.

“Pia zikilingana hapo inaangaliwa mechi zao mbili walizokutana, nani alipata mabao mengi, zikilingana tunakwenda kuangalia nani alifunga mabao mengi ugenini, zikilingana sehemu zote inabidi zikutanishwe tena kucheza ili kupata wa juu.

“Mkanganyiko uliojitokeza kati ya Kagera Sugar na Stand United, ilikuwa katika utofauti wa mabao, baada ya watu wetu  wa data kupitia upya wakabaini  kulikuwa na makosa katika kuingiza matokeo ya mechi ya Mei 16, iliyozikutanisha timu hizo,” alisema Wambura.

Alieleza kuwa katika mechi hiyo, Kagera Sugar ilifungwa mabao 3-1, lakini takwimu zilizoingizwa zilikuwa zinaonyesha  Kagera ililala  mabao 3-0.

 Alisema baada ya marekebisho hayo, Kagera  Sugar itacheza  mechi ya mtoano  Juni 2, mwaka huu dhidi ya Pamba FC, kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza na mchezo wa marudiano utakuwa Juni 8, Kaitaba, Kagera.

Kwa upande wa Mwadui FC, watakuwa wageni wa Geita Gold FC kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita na mechi ya marudiano itachezwa Juni 8, mwaka huu katika Dimba la Mwadui Complex, Shinyanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles