NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene, ameangushwa na Kimwei Mhita (27) katika kinyang’anyiro cha kura za maoni za kumtafuta Mwenyekiti wa Mtaa wa Masaki atakayewakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Waziri huyo ambaye alikuwa anatetea kiti hicho ambacho ameshikilia kwa muda mrefu, amejikuta akiangushwa mwishoni mwa wiki na mwanasiasa huyo kijana ambaye hana umaarufu mkubwa katika medani ya siasa za chama hicho akilinganishwa na waziri huyo.
Mhita alishinda nafasi hiyo ya uenyekiti wa mtaa kwa kupata kura 119 huku Waziri Mbene akiambulia kura 27.
MTANZANIA ilipomtafuta Waziri Mbene kupata maoni yake kwa kuangushwa katika uchaguzi huo, simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu, pia hakuweza kujibu.
Ujumbe wa simu uliotumwa na MTANZANIA ulisomeka hivi: “Mheshimiwa habari za asubuhi naitwa … ninaomba ufafanuzi wa ushiriki wako katika Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Masaki.
“…kuna taarifa kuwa umeshiriki kuwania uenyekiti wa mtaa na kuangushwa na kijana, je ni kweli?”
Mbene ni mbunge wa kuteuliwa na Rais Kikwete katika vipindi viwili tofauti. Kwa mara ya kwanza aliteuliwa kuwa mbunge katika Bunge la tisa na baadaye aliteuliwa tena na kuwa Naibu Waziri wa Fedha.
Baada ya kipindi cha miezi kadhaa, katika mabadiliko aliyoyafanya Rais Kikwete, alimhamisha wizara na kumpeleka kuwa Naibu Waziri Viwanda na Biashara.
Agosti 24 mwaka huu, Kamati ya Siasa ya CCM mkoani Mbeya, iliagiza Mbene aitwe kuhojiwa akidaiwa kuhusishwa na vurugu za siasa katika Wilaya ya Ileje.
Mbene ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alikuwa akilalamikiwa kutumia siasa za kukigawa chama kwa kujenga makundi ndani ya chama hicho.
Uamuzi wa kuitwa kwa Mbene uliwekwa wazi na Katibu Mwenezi wa CCM mkoani Mbeya, Bashiru Madodi, aliyesema uamuzi huo ulifikiwa kwenye vikao vya kamati za siasa vilivyojadili maadili na nidhamu katika mojawapo ya wilaya mkoani humo, kati ya Agosti 22 na 23 mwaka huu.
Hivi sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo katika mchakato wa kura za maoni kuwapata wagombea wake wataoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.