27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu kugawa bodaboda 200

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

NA ELIYA MBONEA-ARUSHA

VIJANA 200 kutoka kata 25 za Halmashauri ya Jiji la Arusha, wanatarajiwa kukabidhiwa bodaboda walizopewa kwa mkopo usio na riba wala dhamana ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Awamu hiyo ya kwanza ya mgawo wa pikipiki 200 zenye thamani ya Sh milioni 400 zikiwa na bima kubwa, zitakabidhiwa kwa vijana hao na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Desemba 3 jijini hapa.

Akizungumza wakati wa mkutano na vijana wa bodaboda pamoja na wadau wengine wa maendeleo jijini hapa jana, Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo, alisema kila kata itatoa vijana wanane watakaokabidhiwa pikipiki hizo.

Gambo alisema mpango huo wa Serikali umelenga kuwakwamua vijana kiuchumi kwa kuwawezesha kupata pikipiki bila riba wala dhamana.

Alisema mpango huo wa kuwapatia pikipiki ulikuja baada ya kukutana na waendesha bodaboda hao na kuwasikiliza malalamiko yao, ambao moja ya kero yao kubwa ilikuwa ni kutozwa fedha nyingi na wamiliki wa bodaboda hizo.

“Nimekuwa nikiona jinsi mnavyojituma kutafuta riziki. Lakini hamthaminiki, kazi hii imedharaulika, muda umefika kwa kazi hii kuwa ya heshima mbele ya jamii.

“Kila kijana aliyepo katika biashara hii ataweza kumiliki pikipiki yake na sio kuendesha pikipiki za watu wengine, ambao wamekuwa wakiwanyonya kwa kuwatoza fedha nyingi huku wao wakiendelea kuneemeka.

“Kundi hili limetumiwa kwa masilahi ya watu wachache kwa kuwa wamekuwa wakipewa pikipiki kwa faida kubwa na mmiliki anapokea fedha zaidi ya mara mbili ya bei ya kununulia pikipiki,” alisema Gambo.

Kutokana na changamoto hizo, alisema mkoa uliona ni vyema kuwajengea uwezo vijana kwa kuwapa mafunzo na pikipiki watakazotakiwa kurejesha kiasi cha fedha halali iliyonunulia pikipiki na baada ya kurejesha mkopo kijana atamilikishwa chombo husika.

Gambo alisema ugawaji wa pikipiki hizo utazingatia kata zilizopo katika jiji hilo na kwamba ugawaji wa awamu ya pili utafanyika kadiri ya mahitaji.

“Tumeweka usimamizi makini kwa watakaopata pikipiki ili warejeshe  fedha  kama inavyotakiwa na tununue pikipiki nyingine kwa vijana, na hatimaye tuwafikie vijana wote wenye uhitaji wa kumiliki na kufanya biashara ya bodaboda,” alisema Gambo.

Kwa upande wake, mmoja wa madereva wa bodaboda, Serafini Shirima kutoka Kata ya Levolosi, alishauri kuundwa kwa kamati ya mpito itakayosimamia na kuratibu mchakato mzima wa vijana watakaoanza kupewa pikipiki hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles