31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatenga bil. 5/- za vifaa kwa wajawazito

Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Na AMINA OMARI – KOROGWE

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetenga Sh bilioni 5 za kununua vifaa vya kujifungulia vitakavyosambazwa katika hospitali na vituo vyote vya afya kwa matumizi ya wajawazito.

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu wakati wa harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya cha Majengo kilichopo wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Alisema kuwa vifaa hivyo vitasambazwa katika hospitali zote nchini ili wajawazito wanaofika katika vituo hivyo wavitumie bila ya kutozwa tozo zozote.

Ummy alisema kuwa lengo la Serikali ni kuona namna bora ya kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga inapungua, hivyo kuwapo kwa vifaa hivyo kutarahisisha utoaji wa huduma.

“Tunatoa kipaumbele katika afya ya mama, hasa afya ya uzazi, hivyo vifaa tayari tumeshanunua kilichopo sasa ni kuweka utaratibu mzuri wa kuvisambaza viweze kuwafikia walengwa kwa wakati,” alisema waziri huyo.

Aidha alibainisha kuwa nia ya Serikali ni kuboresha vituo 100 vya afya nchi nzima ili kuhakikisha huduma ya afya inapatikana kwa wakati.

“Lengo la Serikali ni kuboresha sekta ya afya nchi nzima na labda leo niseme kwamba jengo mlilolianzisha la ghorofa tatu la Kituo cha afya hapa Korogwe ghorofa ya kwanza ninategemea kujengwe chumba cha kisasa cha upasuaji, wodi za wazazi na maabara ya kisasa na haya ndiyo malengo yetu,” alisema waziri huyo.
Katika hatua nyingine,  Waziri Ummy aliwataka wahudumu wa afya kote nchini kuhakikisha wanavaa vitambulisho ambavyo vitakuwa na majina yao kamili ili kuepuka malalamiko ya kuhusika na kutoa lugha chafu kwa wagonjwa.

Alisema kuwa ni lazima kila muuguzi ahakikishe anapotoa huduma awe amevaa kitambulisho ili pale inapotokea ametoa huduma mbovu, iwe rahisi kwa mlalamikaji kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel, alisema ameridhishwa na namna ambavyo wananchi wamehamasika na wamekubali kuyatafuta maendeleo kwa kushirikiana na Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles