Na MWANDISHI WETU-DAR ES SAALAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka mawaziri watumie madaraka yao kwa manufaa ya taifa na kamwe wasiyatumie kama fursa ya kujitajirisha wao binafsi.
Hayo aliyasema Dar es Salaam jana alipozungumza na baadhi ya mawaziri, manaibu na makatibu wakuu katika kikao.
Alisema Rais Dk. John Magufuli amesisitiza kwamba amewateua ili wafanye kazi na na wasitumie madaraka waliyopewa kwa maslahi yao binafsi.
“Madaraka haya ya uwaziri si fursa ya kujipatia utajiri, tunatakiwa tufanye kazi kwa weledi, uadilifu, bidii na uaminifu mkubwa kuondoa kero za wananchi kwa wakati,” alisema.
Alisema mawaziri na manaibu waziri wazingatie katiba ya nchi, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali katika utekelezaji wa majikumu yao ya kila siku.
Aliwataka mawaziri hao kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/21.
Pia utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na ahadi alizozitoa Rais Dk. Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.
Waziri Mkuu aliwaagiza mawaziri wahakikishe wanakwenda kufanya ufuatiliaji wa tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao.
Pia amewataka mawaziri hao wakasimamie kwa ukamilifu ukusanyaji wa mapato na kuanzisha vyanzo vipya vya ukusanyaji na kudhibiti mianya ya upotevu.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka mawaziri hao wakapunguze urasimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali kwa sababu wananchi wanahitaji kuhudumiwa kwa wakati.
Mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Suileiman Jaffo na manaibu wake, Joseph Kandege na George Kakunda, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu wake Dk. Faustine Ndugulile.