ADDIS ABABA, ETHIOPIA
MWENYEKITI wa Chama kinachowakilisha kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia cha Oromo People’s Democratic Organisation (OPDO), DK. Abiy Ahmed anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia.
Hatua hiyo inatokana na kuchaguliwa kuongoza muungano tawala wa Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front EPRDF unaohusisha vyama vikubwa vinne na ambao unadhibiti Bunge na Serikali.
Ahmed alichaguliwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Serikali na atachukua wadhifa huo kutoka kwa Hailemariam Desalegn aliyetangaza ghafla kujiuzulu mwezi uliopita.
Taifa hilo kwa sasa liko katika hali ya dharura iliyotangazwa kwa ajili ya kumaliza maandamano yanayoongozwa na Waoromo takriban miaka mitatu dhidi ya Serikali.
Dk. Ahmed (42), ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa kumrithi Desalegn, anatazamwa na wengi kama mwenye kuzungumza kwa uwazi, ujuzi na uzoefu, na mwenye kukumbatia uongozi wa kushirikisha wote.
Jina lake likitarajia kuwasilishwa Bungeni leo tayari kupigiwa kura na hivyo kuwa mwislamu wa kwanza kuongoza Ethiopia, Ahmed anaaminika kuwa na ufuasi mkubwa miongoni mwa vijana wa Kioromo na pia katika jamii nyingine.
Lakini wakosoaji wake hata hivyo wanasema ni mtu wa ndani katika chama na hivyo hakuna matumaini kwamba matakwa ambayo yamekuwa yakiitishwa na waandamanaji kutatuliwa.