31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu aagiza wafugaji waelimishwe

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amefungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo na ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ishiriki kikamilifu katika kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

“Hakikisheni wafugaji wanaelimishwa na kuhamasishwa kufuga kulingana na maeneo waliyonayo. Halmashauri nazo zihamasishe ufugaji ambao hautachochea migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Jumanne, Septemba 7, 2021 baada ya kufungua mkutano huo wa siku mbili unaofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinashirikiana na wadau wa sekta binafsi wakiwamo wafugaji katika kutenga, kupima, kusimamia na kuendeleza maeneo ya malisho pamoja na kuwahamasisha wafugaji waboreshe mifugo yao ili kuongeza tija kwenye uzalishaji.

“Viongozi na Watendaji wa Serikali hakikisheni mnashirikiana kwa karibu na sekta binafsi wakiwemo wafugaji katika kuwawezesha kuwekeza na kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo majosho, malambo, maeneo ya malisho na visima vya maji,” amesema.

Waziri Mkuu ameeleza kuwa uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za mifugo uimarishwe ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo sambamba na kuwahamasisha wafugaji kutumia mifugo bora iliyofanyiwa tafiti.

Amesema huduma za ugani ziimarishwe kwenye sekta ya mifugo ili wafugaji wapate mbinu bora za ufugaji pamoja na kuimarisha masoko ya mifugo kwa lengo la kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao kwa bei nzuri.

Majaliwa  ametoa wito kwa jamii ya wafugaji kuacha tabia ya kuwapa watoto kazi ya kuchunga mifugo badala yake wajikite kuwapatiaelimu bora kwa manufaa  ya baadae.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema lengo la mkutano huo ni kutoa nafasi kwa wadau wa sekta binafsi kufahamu kwa undani fursa zilizopo katika sekta ya mifugo, kupata uzoefu wa pamoja na kufahamu changamoto na kujadili namna ya kuziondoa.

Ndaki ametoa wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zigharamie na kuwashirikisha wafugaji nchini wahimilishe asilimia 20 ya ng’ombe wanaostahili kuhimilishwa kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano ili kufikia lengo la wizara la kuboresha mifugo milioni tano katika kipindi cha kuanzia 2020 hadi 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles