23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Jenista akagua mifumo ya usalama na afya mgodi wa Shanta

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amefanya ziara katika mgodi wa dhahabu wa Shanta uliopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa lengo kukagua usimikaji wa mifumo ya usalama na afya katika hatua za awali za maandalizi ya uchimbaji madini katika mgodi huo.

Katika ukaguzi huo Jenista amesema ni muhimu kuhusisha wataalamu   usalama wa afya sehemu za kazi ikiwamo migodini katika hatua za ujenzi wa awali wa miundombinu ili waweze kupata ushauri utakaowawezesha kujenga kinyume na Sheria na Kanuni za Usalama na Afya mahali pa kazi.

“Kwetu sisi na wenzangu wa OSHA tutakachojitahidi ni kuendelea kuwapa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ili mbobee kwenye eneo hilo kusudi muondoshe migogoro katika eneo lenu la kazi na ndio maana ninaomba muwaruhusu hapa wawe na tawi la wafanyakazi.

“Lakini tutawasadia pia kukagua na kuangalia mifumo yenu ya usalama na afya kama itaweza kulinda afya za wafanyakazi hususan pale mtakapoanza rasmi uzalishaji kwani tunatambua kwamba shughuli hizi za uchimbaji madini huambatana na vihatarishi vingi vya usalama na afya ambavyo vinahitaji mifumo madhubuti ya kukabiliana navyo,” amesema Jenista.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Mhandisi Alexander Ngata, ametoa wito kwa kampuni kubwa ambazo zinafanya kazi na kampuni saidizi (sub-contractors) kuhakikisha zinazingatia sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi.

Akiwasilisha taarifa yake kuhusu hali ya usalama na afya katika mgodi huo mbele ya Waziri, Mhandisi Ngata ameeleza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikijitahidi kutekeleza matakwa yote ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi kama ambavyo wamekuwa wakielekezwa na wataalam kutoka OSHA.

Aidha,  ametaja  changamoto iliyopo ni kwa kampuni saidizi (sub-contractors) zinayofanya kazi na Shanta ambazo bado hazizingatii utekelezaji wa sheria tajwa.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma, Venance Buliga, amesema wamekuwa wakishirikiana ipasavyo na uongozi wa mgodi huo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya uchimbaji madini katika mgodi huo ambapo wamekuwa wakifanya ukaguzi na kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu namna bora ya kujenga miundombinu inayozingatia afya na usalama wa wafanyakazi.

Menejimenti ya mgodi huo pamoja na wafanyakazi wameeleza kuwa usalama na afya kwa wafanyakazi ni miongoni mwa vipaumbele vya kampuni hiyo.

“Tunafanya kazi kwa kuzingatia misingi mitatu ambayo ni biashara, mahusiano na jamii inayotuzunguka pamoja na afya na usalama wa watu wetu kama kama tulivyoeleza katika taarifa yetu kwa Mheshimiwa Waziri na yeye pamoja na wataalam wa OSHA wamethibitisha hilo walipotembelea sehemu mbalimbali katika mgodi,” amesema Mhandisi Jiten Divecha, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Shanta wa Ikungi Mkoani Singida.

“Kwa masuala ya usalama na afya hapa Shanta tuko vizuri sana, kila sehemu ambayo watu wanafanya kazi masuala ya matumizi sahihi ya vifaa kinga yanazingatiwa ipasavyo na pia wakaguzi wa OSHA huwa wanatutembelea kuangalia namna tunavyofanya kazi na kutushauri kuboresha endapo tunakuwa kinyume na taratibu za usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Ferdinand Cyprian, mfanyakazi wa Mgodi wa Shanta-Ikungi katika kitengo cha upakaji rangi majengo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles