25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri anasa kiwanda cha viroba feki

viroba-fekiJOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM

KIWANDA feki cha kutengeneza konyagi feki na bidhaa zake kimegundulika   Dar es Salaam baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla kuvamia kiwanda hicho.

Tukio hilo lilitokea saa 8:00 mchana jana baada ya Dk. Kigwangalla kwa kushirikiana na Maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA) na Tume ya Ushindani pamoja na Jeshi la Polisi kunasa kiwanda hicho bubu.

Kiwanda hicho kilinaswa kwenye nyumba ya mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la Koku maarufu ‘Mama Kareem’ eneo la Sinza Kijiweni,  Dar es Salaam, kikitengeneza konyagi, viroba na pombe kali ya  smirnoff.

Katika kiwanda hicho pia kulikutwa malighafi mbalimbali zinazotumika kutengenezea bidhaa hizo likiwamo dumu kubwa lililokuwa  limejaa gongo.

Vingine ni  dumu la spirit lita 20, chupa tupu  na zilizojazwa kwa ajili ya kusambazwa, vizibo vya chupa za konyagi na smirnof pamoja na  vifungashio vya aina mbalimbali.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Meneja wa TFDA Kanda ya Mashariki, Emmanuel Alphonce, alisema kiwanda hicho kimebainika baada ya kupata taarifa kutoka kwa majirani wa mwanamke huyo ambao walitilia shaka mwenendo wa biashara alizokuwa akizifanya.

“Ni kweli tumekamata kiwanda kinachotengeneza konyagi feki huko Sinza lakini tunaendelea na msako na tutatoa taarifa ya pamoja baadaye.

“Kiwanda hicho kilikuwa kinatengeneza vinywaji hivyo kwa kutumia ‘spirit’ ambayo inachanganywa na gongo.

“Bidhaa zilizokamatwa ni pamoja na dumu kubwa la kuhifadhia pombe, spirit lita 20, chupa tupu na zilizojazwa, vizibo   na  vifungashio mbalimbali,” alisema Alphonce.

Taarifa ya Dk. Kigwangala aliyoisambaza kupitia mitandao ya  jamii jana, ilisema Jeshi la Polisi limewatia mbaroni watu wawili ambao inasemekana ni wafanyakazi wa kiwanda hicho.

Alisema pia kuwa  linamsaka mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Yusuf Abdul Kalambo.

Wakati hayo yakiendelea, Novemba 8, mwaka huu, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema Serikali inazishauri sekta binafsi kuanzisha viwanda vya kutengeneza gongo kwa viwango vya usalama na ubora.

“Faida za   gongo zinafahamika, wataalamu wangu wana uwezo wa kujua faida ya kinywaji hiki tatizo letu ni usalama, kwa hiyo mimi nitawaelekeza wataalamu wangu waje kwenye jimbo lako kuhakikisha kile kinywaji kitengenezwe salama,” alisema Mwijage wakati akijibu baadhi ya maswali ya wabunge.

Wakati huohuo, jana gazeti hili liliripoti kuwa mkulima wa Kijiji cha Kingo Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Kalama Kioli alikutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake baada ya kunywa viroba vya konyagi.

Mkulima huyo anadaiwa alikunywa pombe hiyo alipokuwa kwenye sherehe kijijini hapo usiku wa kuamkia Novemba 8 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles