23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein asaini sheria ya mafuta, gesi

pg-4Na MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, jana amesaini sheria ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ya Zanzibar.

Mbali ya kusaini sheria hiyo, amewapiga kijembe wanaoikosoa sheria hiyo kuwa ni wachoyo na wasioitakia mema Zanzibar.

Dk. Shein aliwaambia viongozi na waandishi wa habari kuwa sheria hiyo namba 6 ya mwaka 2016, inaipa Zanzibar mamlaka ya kisheria ya kuendeleza rasilimali ya mafuta na gesi asilia.

Alisema kitendo cha kutia saini sheria hiyo, hakijavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano kama baadhi ya watu wanavyodai.

“Hakuna aliyevunja sheria, anayevunja sheria wala atakayevunja sheria. Lakini kama wao wanadai kutia saini sheria hii ni kuvunja sheria, basi watafute suluhisho la kisheria,” alisema.

Aliwashauri wenye mawazo hayo wakasome vizuri Sheria ya Mafuta Namba 21 ya 2015 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imeweka msingi imara wa kisheria wa kutambua rasilimali ya mafuta na gesi asilia ni miongoni mwa mambo yaliyoorodheshwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yanahitaji usimamizi bora na imara wa kisheria.

Alisema sheria hiyo imeainisha mambo makuu matatu ambayo kwanza ni kuwa shughuli zote za mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania Bara zitasimamiwa na taasisi zilizoanzishwa ndani ya sheria namba 21 ya 2015.

Sheria hiyo inatamka pia kuwa shughuli zote za mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania Zanzibar zitafanywa na taasisi zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania Zanzibar.

Kuhusu mapato yatokanayo na shughuli hizo, Dk. Shein alisema sheria inatamka upande wa Tanzania Bara mapato yatatumiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa faida ya Tanzania Bara wakati kwa upande wa Tanzania Zanzibar yatatumiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa faida ya Zanzibar.

“Kila upande ulishiriki kikamilifu katika mchakato huu. Tulishauriana kwa kina viongozi na tukapata ushauri wa kutosha kutoka kwa wanasheria wetu wakuu hadi kufika bungeni,” alisema Dk. Shein.

Alisema anatambua sheria hiyo ni mpya na anaelewa changamoto ambazo zinaweza kutokea, lakini akatoa wito kwa wananchi kuiunga mkono na kushirikiana na Serikali.

“Mafuta ni jambo kubwa katika maendeleo, pia yasipotumika vyema yanaweza kuitikisa nchi,” alisema Dk. Shein.

Aliwatahadharisha wananchi kutegemea mafanikio ya haraka kutoka sekta hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles