Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Baraza la wazee wa Chama Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limetoa wito kwa serikali kuangalia upya sera ya wazee ili wapatiwe pensheni zao mara tu wanapostaafu kutokana na kuwepo kwa ucheleweshwaji wa posho hizo jambo linalosababisha wengine kufariki bila kupatiwa stahiki zao.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Oktoba Mosi, katika siku ya wazee duniani na Katibu Mkuu wa Baraza hilo Rodrick Lutekamba, ambapo kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Wazee ni Hazina ya Hekima na Busara tusikilizwe, tuheshimiwe, tuthaminiwe na tulindwe’ .
Amesema wameitaka serikali kuwasikiliza wazee kwa sababu wanazo busara na hekima ambazo zikisikilizwa na kutumika vyema vitaipeleka nchi sehemu nzuri.
“Wazee wanakumbana na changamoto nyingi zikiwamo kutopata huduma nzuri za afya kutokana na kukosa madawa wanapoumwa, tunasikitika kuona serikali inatumia fedha nyingi katika kufanya chaguzi za marudio ilihali zingetumika katika kuboresha miundombinu ya afya ili tukapata huduma nzuri tunapoenda hospitalini,” amesema.
Naye mwenyekiti wa Baraza hilo, Hashim Issa, amesema wanaishauri Serikali kuwepo na viti maalumu kwa ajili ya wazee bungeni na hii itasaidia kufikisha kwa haraka kero zao na zikatatuliwa.