NA BEATRICE MOSSES
UKOSEFU wa walimu wa hesabu umewafanya wazazi wa watoto wanaosoma katika Shule ya Sekondari Bagara wilayani Babati kuunda kamati ya kuboreshai taaluma shuleni hapo.
Katibu wa Kamati hiyo, Dismas Kokumo alipozungumza na MTANZANIA juzi alisema wazazi wamekubaliana kuchanga Sh 25,000 kila mmoja kwa ajili ya kumlipa mwalimu wa somo hilo.
Alisema vilevile wamekubaliana kutoa Sh 5,000 kila mmoja kwa mwaka kwa ajili ya kununu karatasi.
“Baada ya kuona kuna tatizo la walimu wa hesabu tulikubaliana wazazi tuchangie Sh 25,000 kwa ajili ya kumlipa mwalimu kwa mwaka kila mwanafunzi na Sh 5000 za
karatasi,’’ alisema Kokumo.
Alisema wameweka utaratibu wa wanafunzi kupewa mazoezi na mwalimu huyo kujua kama wanachofundishwa wanakielewa .
Kokumo alisema kamati iliyochaguliwa na wazazi ndiyo inaratibu suala la kumlipa mwalimu baada ya michango kuchangwa na fedha kuhifadhiwa katika Benki ya CRDB.
“Kupatikana kwa mwalimu wa hesabu kumesaidia kuongeza ufaulu katika shule hii maana tumetoka zero 80 mwaka uliopita hadi zero tano ambazo ni za wale watoro,’’ alisema.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Emmanuel Dahaye, alikiri wanafunzi kuchangishwa michango kwa ajili ya mwalimu wa hesabu baada ya uamuzi wa wazazi.
Alisema kufanya hivyo kulitokana na waraka wa elimu uliotolewa na TAMISEMI uliowataka kufanya hivyo inapobidi baada ya kukubaliana na wazazi.
"Ni nyaraka ambazo tulipewa kwamba shule inapokuwa na tatizo fulani wazazi wenyewe wafanye uamuzi, wafanye mchanganuo na hizo shughuli zote ziratibiwe na wazazi wenyewe," alisema Dahaye.
Alisema baada ya kukubaliana waliamua kila mwanafunzi achangie Sh 12,500 kwa muhula mmoja lakini hata ambao hawachangii kwa wakati hawawafukuzwi bali wanavumiliwa.