Na DERICK MILTON – SIMIYU
SIKU moja baada ya kuripotiwa habari juu ya kuibiwa kwa mashine ya kupima magonjwa ya ndani mwa mwili wa binadamu (ultrasound) katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi ya Somanda, Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga, ameagaza wafanyakazi wa hospitali hiyo kujichangisha na kuinunua.
Katika kikao chake na watumishi wa hospitali hiyo, Kiswaga ametoa siku saba kwa watumishi wote kuchanga kulingana na mishahara kwa kila mmoja kuhakikisha wananunua mashine hiyo.
Kikao hicho ambacho kilifanyika jana katika ukumbi wa hospitali hiyo, Kiswaga alimtaka Mganga Mkuu wa Halmashuari hiyo, Mkurugenzi wa Halmashuari kuhakikisha ikifika Agosti 21, wapeleke mashine hiyo Ofisini kwake.
“Kwa kuwa mashine hii iliibiwa mchana na ikaibiwa na vifaa vyake vyote, inaonyesha kuwa walihusika ni wataalamu na kwa maana hiyo watumishi wote 137 wa hospitali hii mnahusika na wizi huu, hivyo nyie ni watuhimiwa wa kwanza wa wizi huu.
“Kila mmoja kuanzia kwa Mganga Mkuu wa Halmashuari mtachangia kulingana na kila mtu na mshahara wake, nataka ndani ya siku saba nikabidhiwe hiyo mashine, ambaye atagoma kuchangia huyo itakuwa halali yangu,” alisema Kiswaga.
Pia alisema kuwa watumishi 17 ambao walikamatwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi, kesi yao itaendelea kufanyiwa kazi, huku akimtaka Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kukamilisha uchunguzi unakamilika haraka.
Aidha Kiswaga alimtaka Ofisa Utumishi wa Halmashuari hiyo kuorodhesha majina yote ya watumishi hao kwenye karatasi kisha kumpatia kwa ajili ya kuangalia nani atakaidi kuchanga ili mashine hiyo inunuliwe.
Aidha alisema tabia ya wizi katika hospitali hiyo imekuwa sugu ambapo wahusika wakuu wamekuwa watumishi wake, hali ambayo alieleza hawezi kuivumilia kama kiongozi wa Wilaya.
“Siyo mara ya kwanza kutokea wizi kwenye hospitali hii, mlihusika na wizi wa darubini (Microscope) ambapo baadaye ilipatikana ikiwa juu ya mti imeninginizwa, mkaiba tena mashine ya kufulia nguo ambayo mpaka sasa haijapatikana na leo tena Ultrasound hii haiwezekani na wala haikubaliki,” aliongeza Kiswaga.
Alisema kitendo hicho ni uhujumu uchumi hivyo watumishi wote lazima wahusike katika kuhakikisha mashine hiyo inarudishwa kwa gharama zao.
Kiswaga alisema yuko tayari kufukuzwa kazi kwa hatua yeyote ambayo atachukua kwa watumishi hao ikiwa watashindwa kuhakikisha wanarudisha mashine hiyo kupitia michango yao ndani ya muda ambao ametoa.
Awali akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Halmashuari, Merkzedeck Humbe, alisema kitendo hicho ni fedhea kwa halmashuari na Serikali hivyo alisema hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika.
“Mashine hii haiwezi kuibiwa na mtu yeyote kutoka nje bila ya kuwepo kwa ushirikiano kutoka kwa watu wa ndani, lazima wahusika wapo humu humu, kama ambavyo mlirudisha darubini basi fanyeni hivyo kwa mashine hii,” alisema Humbe.
Awali akitoa taarifa ya wizi huo Mganga Mkuu wa Halmashuari, Mike Mabimbi, alisema mashine hiyo iliibiwa Agosti 5, majira ya mchana ikiwa kwenye wodi ya akina mama wajawazito hospitalini hapo.
Mabimbi alisema baada ya kupata taarifa za wizi huo walitoa taarifa polisi ambapo, watumishi 17 walikamatwa na wamehojiwa ambapo uchunguzi dhidi yao bado unaendelea.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya ametaifisha pamba inayodaiwa kuwa ya magendo ikiwa ni siku mbili baada ya kukamatwa kwa gari aina ya scania yenye namba za usajili T917 BCN ikiwa na pamba tani zaidi ya 20.
Pamba hiyo ilikamatwa katika Kijiji cha Dutwa Wilayani Bariadi mkoani Simiyu, Agosti 12, saa tano usiku, ikisafirishwa bila kibali maalumu huku ikiwa haijulikani wapi inapelekwa na wapi imenunuliwa.
“Baada ya wahusika kushindwa kujitokeza, sasa kama Mkuu wa Wilaya nachukua uamuzi wa kuitaifisha pamba hii na tunaenda kuiuza kwenye viwanda vya kuchambua pamba leo hii na fedha zote zitapelekwa kununua vifaa vya kukamilisha ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Simiyu,” amesema Kiswaga.