Na SAMWEL MWANGA
WAZAZI na walezi wa watoto albino katika Wilaya ya Bariadi wamebuni mbinu mpya ya kuwapaka rangi nyeusi watoto wao kwenye ngozi na nywele kuwalinda na vitendo vya ukatili na hata tishio la kuuawa.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Dutwa wilayani Bariadi, George Epafra alikuwa akizungumza wakati wa kutambulisha mradi wa kukomesha mauaji ya albino unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Mass Media katika wilaya hiyo.
Epafra alisema mbinu hiyo imeibuka baada ya baadhi ya vituo vya kulelea watoto albino kufungwa na serikali na watoto hao kukabidhiwa kwa wazazi wao kwa ajili ya kuendelea kuwalea.
Kwa sababu hiyo jukumu la kuwalinda wasiweze kufanyiwa vitendo vya ukatili limeachwa kwa wazazi.
Alisema wazazi wamekuwa wakiwapaka masizi meusi na wengine wakitumia dawa ya piko ambayo hutumika kuweka katika nywele ili kuficha uhalisia wa nywele zao na ngozi kwa kuhofia ya kuuawa na watu wenye imani potofu za ushirikina.
“Hivyo watoto wengi sasa wamerudishwa majumbani na idadi kubwa wako vijijini.
“Hivyo katika kuwalinda dhidi ya ukatili na kuuawa, wazazi na walezi wao wameanza kuwapaka masizi meusi sehemu mbalimbali za miili yao huku nywele zikipakwa dawa ya piko zionekane ni nyeusi,”alisema.
Alisema wazazi wengi wamekuwa katika hali ya kutapatapa huku wengine wakiendelea kuiomba Serikali kuwatatulia kero zinazowakabili watoto wao waishi kwa uhuru.
Epafra alisema baadhi wanataka wapatiwe elimu baada ya kupewa misaada ambayo siyo endelevu katika mapambano dhidi ya ukatili.
Mratibu na Msimamizi wa Mradi huo, Frank Kasamwa alisema lengo la mradi ni kubadilisha mtazamo wa wananchi kuwa viungo vya albino vinasababisha tajiri.
“Tunataka tuibadilishe jamii juu ya dhana hii ya kuwaua albino kuwa viungo vyao vinamfanya mtu awe na mali au utajiri hasa katika kuelekea uchumi huu wa viwanda.
“Ni lazima tuondokana na hizi mila potofu tumwone mtu mwenye ulemavu huo ni binadamu wa kawaida na kupata mali au utajiri ni lazima tufanye kazi,”alisema.
Alisema mradi huo ambao umepata fedha kutoka Foundation For Civil Society (FCS) utatekelezwa katika wilaya za Bariadi, Maswa na Itilima.
Vilevile watawahamasisha wataalamu wa afya kukutana na wataalamu wa tiba asili kuweka mikakati ya pamoja katika kuwalinda albino na kuepuka ramli chonganishi.