31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAKIMBIZI 302 KUTOKA BURUNDI WAANZA KUREJESHWA KWAO

Na EDITHA KARLO-KIGOMA

WAKIMBIZI 301 kati ya 12,000 wa Burundi wanaoishi katika kambi ya wakimbizi ya Nduta  wilayani Kibondo wameanza kurejeshwa kwao   kwa awamu.

Kurejeshwa kwa wakimbizi hao kunatokana na makubaliano baina ya pande tatu ambazo ni Serikali ya   Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbuzi   (UNHCR) kujiridhisha kuwa   Burundi kwa sasa ina amani.

Akizungumza   baada ya kuwakabidhi wakimbizi hao kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa   Burundi katika eneo la Mamba mpakani mwa Tanzania na Burundi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga, alisema wanaoanza kurejea kwa siku ya kwanza ni familia 97 na awamu nyingine watawarejeshwa wiki ijayo.

Alisema katika kikao wiki iliyopita cha pande zote tatu, waliamua kuanza kuwarejesha wakimbizi hao na kubainisha kuwa serikali ya Tanzania itawakabidhi kwa Serikali ya Burundi wakimbizi wa awali 301 na hadi kufikia mwishoni mwa Septemba watakuwa wamewarejesha wengine 6,000 wengine ni Oktoba na Desemba.

Mkuu huyo wa mkoa aliwaomba wakimbizi hao kuanza kujitokeza kurejea mapema na wasisubiri kuondoka kwa mrundikano hali inayoweza kuwapa ugumu katika usafirishaji.

Mratibu wa Wakimbizi Kanda ya Kigoma, Tony Laizer, alisema kwa sasa kuna wakimbizi 127,715 walioomba hifadhi na kati yao 12,000 wameomba kurudishwa kwao hivyo kuchelewa kuwarejesha mapema kulitokana na hali ya usalama kutokuwa nzuri baada ya kuibuka  vitendo vya vurugu mara kwa mara.

“Hatua hii ya  kuwarejesha itasaidia kuwapo  usalama na amani katika kambi kutokana na wakimbizi wengi kuomba kurejeshwa kwao… ninaamini hatua hii itasaidia kuwapa nguvu wakimbizi wengine kuendelea kuamini kuwa nchini kwao kuna amani na hatua hii itakuwa muendelezo kwa kambi zote,” alisema.

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi  ya Burundi, Therence Ntahiraja alisema wao kama viongozi wa Burundi wamejipanga ipasavyo kuwapokea wakimbizi kwamba kila atakayerejea atakabidhiwa mali zake walizokuwa nazo mwanzoni na kupewa eneo ya kufanyia shughuli za kuendesha maisha.

Alisema kwa sasa Burundi ina amani na kuwaomba wakimbizi wote warejee nchini kwao   waweze kufanya shughuli za maendeleo na uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles