29.9 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO ALBINO WAPAKWA MASIZI MEUSI WASIUAWE

Na SAMWEL MWANGA

WAZAZI na walezi wa watoto albino katika Wilaya ya Bariadi   wamebuni mbinu mpya ya kuwapaka rangi nyeusi watoto wao kwenye ngozi na nywele  kuwalinda na vitendo vya ukatili na hata tishio la kuuawa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Dutwa wilayani Bariadi, George Epafra alikuwa akizungumza wakati wa kutambulisha mradi wa kukomesha mauaji ya albino unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Mass Media katika wilaya hiyo.

Epafra alisema mbinu hiyo imeibuka baada ya baadhi ya vituo vya kulelea watoto albino kufungwa na serikali na watoto hao kukabidhiwa kwa wazazi wao kwa  ajili ya kuendelea kuwalea.

Kwa sababu hiyo   jukumu la kuwalinda  wasiweze kufanyiwa vitendo vya ukatili limeachwa kwa wazazi.

Alisema wazazi wamekuwa wakiwapaka masizi meusi na wengine wakitumia dawa ya piko ambayo hutumika kuweka katika nywele ili kuficha uhalisia wa nywele zao na ngozi kwa kuhofia ya kuuawa na watu wenye imani potofu za ushirikina.

“Hivyo watoto wengi sasa wamerudishwa majumbani na idadi kubwa wako vijijini.

“Hivyo   katika kuwalinda dhidi ya ukatili  na kuuawa, wazazi na walezi  wao wameanza kuwapaka masizi meusi  sehemu mbalimbali za miili yao huku nywele zikipakwa dawa  ya piko zionekane ni nyeusi,”alisema.

Alisema wazazi wengi wamekuwa katika hali ya kutapatapa huku wengine wakiendelea kuiomba Serikali kuwatatulia kero zinazowakabili watoto wao  waishi kwa uhuru.

Epafra alisema  baadhi wanataka wapatiwe elimu baada ya kupewa misaada ambayo siyo endelevu katika mapambano dhidi ya ukatili.

Mratibu na Msimamizi wa Mradi huo, Frank Kasamwa alisema   lengo la mradi   ni kubadilisha mtazamo wa wananchi kuwa viungo vya albino vinasababisha tajiri.

“Tunataka tuibadilishe jamii juu ya dhana hii ya kuwaua albino kuwa viungo vyao vinamfanya mtu awe na mali au utajiri hasa katika kuelekea uchumi huu wa viwanda.

“Ni lazima tuondokana na hizi mila potofu tumwone mtu mwenye ulemavu huo ni binadamu wa kawaida na  kupata mali au utajiri ni lazima tufanye kazi,”alisema.

Alisema   mradi huo ambao umepata fedha kutoka Foundation For Civil Society (FCS) utatekelezwa katika wilaya za Bariadi, Maswa na Itilima.

Vilevile  watawahamasisha wataalamu wa afya kukutana na wataalamu wa tiba asili   kuweka mikakati ya pamoja katika kuwalinda albino na kuepuka ramli chonganishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles