Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unalaani vikali kuongezeka kwa tabia ya matumizi ya nguvu kunakofanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi wakati wanapokuwa kazini.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo ole Ngurumwa, alisema jana kuwa mtandao huo hauungi mkono kwa namna vitendo vya jinai vinavyofanywa na wananchi wa kawaida, viongozi wastaafu na maofisa wa polisi ambao wamekuwa wakitumia nguvu wanapokuwa kazini.
Alisema mtandao unatambua kwa ukamilifu kwamba Jeshi la Polisi nchini linafanya kazi kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha na kazi zake zilizoainishwa katika kifungu cha 5 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na huduma saidizi.
“Kifungu hiko kinaeleza kwamba Jeshi la Polisi litafanya kazi katika kulinda amani, kusimamia sheria na utulivu, kuzuia na kugundua uhalifu, kukamata na kuwaweka kizuizini wahalifu, ulinzi wa mali na kwa ajili ya utendaji wa kazi zote kama hizo na watakuwa na haki ya kubeba silaha.
“Zaidi ya hayo, THRDC inatambua kazi kubwa inayofanywa na maofisa wa polisi hasa juu ya usalama wa raia na mali zao na kwa hiyo mtandao unawatambua kua nao ni watetezi wa haki za binadamu,’’ alisema ole Ngurumwa.
Alisema ikumbukwe hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la matukio ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi na wengine hata kuwatolea bunduki wananchi.
Pia Mei 15 mwaka huu, askari mwenye silaha akiwa ameambatana na askari mwingine na wafanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya PBEL, alifyatua risasi hewani kwa madai kwamba alikua na lengo la kumlazimisha Naibu Waziri wa zamani wa Fedha, Adam Malima, kutii amri halali ya polisi.
“Kutokuelewana huko kati ya maofisa wa polisi na Adam Malima kulisababishwa na madai ya maegesho ya gari katika sehemu isiyoruhusiwa.
“THRDC haipingi au kuidhinisha madai ya maegesho mabovu ya magari bali inasikitishwa na namna ambayo maofisa wa polisi wamekua wakitumia nguvu kubwa kwa watuhumiwa,’’ alisema.
Alisema mtandao huo pia unalaani tabia ya viongozi wastaafu kutotii amri za polisi kwa kigezo cha hadhi na nafasi zao.
Ikumbukwe kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria na maofisa wa polisi lazima wapewe ushirikiano wanapokamata mhalifu, alisema.
Alisema THRDC inaona kitendo cha polisi kilikua kinyume cha sheria kwa sababu sheria iko wazi juu ya mazingira ya kumkamata mtuhumiwa na jinsi ambavyo ofisa wa polisi anaweza kutumia nguvu katika kutekeleza majukumu yake.
Mtandao huo pia umepinga na kulaani kitendo cha uvamizi wa waandishi wa habari pamoja na viongozi wa CUF waliokuwa katika mkutano Aprili 2, mwaka huu katika Hoteli ya Vina Dar es Salaam.
“Ifahamike kwamba waandishi wa habari na wananchi wengine wana haki ya uhuru wa maoni ambayo ipo kikatiba katika Ibara ya 18 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, 1977.
“Wavamizi hao baada ya kuvamia mkutano huo walianza kuwapiga waandishi na watu wengine waliokuwa katika mkutano huo na hivyo kuwasababishia majeraha ya mwili,’’ alisema.