25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, MUSEVENI WASAINI MRADI BOMBA LA GESI

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni, wametia saini tamko la pamoja la kukamilika  majadiliano ya vipengele vya mkataba kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima  Uganda hadi mkoani Tanga.

Hafla ya kutia saini tamko hilo ilifanyika Ikulu  Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali   na wakurugenzi wa taasisi mbalimbali zinazohusika na mradi huo.

Baada ya kutia saini tamko hilo wataalamu wataandaa mkataba wa mradi kati Tanzania  ambao umepangwa kukamilika katika kipindi cha wiki moja na kuanza taratibu za kuweka jiwe la msingi   kuanza kwa ujenzi wa mradi huo.  

Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Hoima – Tanga wenye urefu wa kilometa 1,443 zikiwamo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania, utagharimu Dola za Marekani bilioni 3.55, unatarajiwa kusafirisha mapipa 200,000 ya mafuta kwa siku na wakati wa ujenzi unatarajiwa kuzalisha ajira kati ya 6,000 na 10,000.

Akizungumza baada ya kutia saini tamko hilo, Rais Magufuli alimshukuru Rais Museveni kwa hatua ambayo Tanzania na Uganda zimefikia katika mradi wa bomba la mafuta   na utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya urafiki na udugu wa  historia uliopo kati ya nchi hizo mbili.

“Huu ni mradi mkubwa, najua Uganda mmepata mapipa bilioni 6.5 ya mafuta huko Hoima na pengine mtapata mengine na sisi pia tunatarajia kupata mafuta kule ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, haya yote tutayapitisha kwenye bomba hili hili.

“Kwa hiyo mimi nakushukuru   Mhe. Museveni na kwa niaba ya Watanzania wote tumefurahi, umetengeneza historia ya Tanzania na Uganda na pia umeimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu, Watanzania hawatakusahau,” alisema Rais Magufuli.

Naye Rais Museveni alimpongeza Rais Magufuli kwa kutia msukumo   kufanikisha mradi huo.

Alisema  mradi utakuwa na manufaa kwa nchi za Afrika Mashariki yakiwamo mashirika ya ndege ambayo yatapata mafuta kwa gharama nafuu.

 “Nimefurahi sana leo (jana), najua kuna kazi kubwa imefanyika hadi kufikia hatua hii, lakini hii pia imeonyesha kuwa na sisi tunaweza,” alisema Rais Museveni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles