33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wateja walalamikia uongozi Azam Mwandege

Said Salim BakhresaNA MwandishiWetu, MKURANGA

WATEJA wanaopeleka kuuza mazao yao ya  matunda na hasa maembe na mananasi ambayo yote ni mazao ya msimu wa kutengeneza juisi, wanalalamika kuhusu upokeaji wa mazao yao na uongozi wa kiwanda  cha Azam kwani wanapata hasara.

Kiwanda hicho ambacho Rais Magufuli alikifungua mwezi uliopita na kukipigia chapuo, kinaonekana kimeanza kuonesha uzembe na sintofahamu nyingi ya namna kinavyofanya kazi na kuanza kutia wasiwasi.

Watu hao wanasema kuwa biashara ilianza vizuri lakini sasa hali si nzuri kwani matunda yao huozea hapo hapo getini kwa ukiritimba unaofanywa na uongozi kwa kuchelewa kupokea mzigo. Sababu ya kucheleweshwa huko haielezwi lakini inakisiwa kuwa  wapokeaji wanataka rushwa kwani watu wengine wa magari yao yanakuja nyuma na kuruhusiwa kuingiza na kupokelewa. Kwa sababu za masilahi ya wauza matunda hao, hawatatajwa  majina kwani kunaweza kutokea zahama.

“Kinachoonekana ni mchanganyiko wa mambo kwani utawala unakosa umakini na vilevile kuna harufu ya rushwa kutokana na upendeleo wa wazi unaofanywa kwa  baadhi ya wafanyabiashara,” anasema muuza matunda mmoja kutoka Muheza, Mkoa wa Tanga.

Kwa wakulima wa matunda wazoefu wanadai hali inayojitokeza kule Mwandege Mkuranga  ni sura kamili ya uendeshaji wa viwanda vya Azam kwani huanza na ari ya kutengeneza juisi ya matunda lakini baadaye hubadilika na kutumia sana kemikali ‘concentrates’ toka nje kwani ni rahisi kutengeneza na hivyo huleta faida kubwa.

“Kuanza kununua matunda mbalimbali ni kudanganya Serikali ili apate vibali na nembo za mamlaka kama TFDA na TBS, lakini haupiti muda huanza kutengeneza juisi za kemikali na hizo hutawala mauzo yao,” alidokeza mwandani huyo.

“Mbaya zaidi viwanda vyake huua mitaji ya watu kwa  kuwatia hasara kwa kufanya matunda yaoze kabla ya kupokea mzigo na hivyo kupata hasara ya kibiashara. Mwaka au msimu unaofuata, wakulima huachana na biashara hiyo,” aliendelea kusema mwandani huyo.

“Ninazungumza hivyo kutokana na yaliyonikuta kama mkulima wa Pugu Kajiungeni ambapo tulishawishika na wenzangu kulima mapasheni kuuza kwa kiwanda cha  Azam na akatutenda vibaya na tumeacha biashara hiyo,” alisema mkulima huyo ambaye hakutaka atajwe jina lake.

Anasema alianza kulima pesheni ‘passion’ halafu maembe, lakini aliacha baada ya kuona kuwa haina faida na kuhamia kulima vitunguu huko Hedaru na Ruvu na anasema ni biashara yenye kipato  kizuri na wana mipango ya kuuza nje bidhaa hiyo.

Anasema vitunguu vinalipa sana na amesikia kule Mbulu wakulima wake wameendelea sana na ana mipango ya kwenda kujifunza huko.

Juhudi za kumwona ofisa yoyote wa Kampuni kutoa maelezo kuhusu tuhuma hizo zimeshindikana na kule Mwandege mambo hayakuwa mazuri walipogundua wanaowatafuta ni waandishi wa habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles