25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kukatikakatika kwa umeme kwayumbisha  viwanda nchini

mitambo-ya-umemeNa Justin Damian

WAKATI Serikali ikisisitiza azma yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, suala la umeme wa uhakika bado linaendelea kuvitesa viwanda vilivyopo ambavyo kwanza ni vichache  na ni vidogo (Light industries).

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA umegundua kuwa umeme wa uhakika bado ni tatizo kwa viwanda  hapa nchini, japo kumekuwa na unafuu ukilinganisha na miaka ya nyuma. Uwezo wa kuzalisha umeme nchini umeongezeka kutoka megawati 1,226.24 Aprili mwaka 2015 hadi megawati 1,461.69 Aprili mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la megawati 235.45 ndani ya mwaka mmoja.

Pamoja na ongezeko hilo, umeme umeendelea kutokuwa wa uhakika, jambo linalotia shaka endapo azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda inaweza kutimia.

Coast Millers ni moja kati ya  viwanda vikubwa  vinavyozalisha unga wa ngano kilichopo jijini Dar es Salaam ambacho uzalishaji wake unategemea sana umeme wa Tanesco. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha unga wa ngano kufikia  metriki tani 300 kwa siku.

Mkuu wa Kitengo cha Mauzo na Masoko wa kiwanda hicho, Vidya Sagar, aliliambia MTANZANIA kuwa, kiwanda hicho kinategemea umeme kutoka Tanesco kwa asilimia mia moja.

Anasema endapo itatokea umeme kukatika, huwalazimu kuzima mitambo na kusimamisha uzalishaji kwa kuwa  matumizi ya jenereta ni gharama kubwa na husababisha hasara.

“Mitambo ya kuzalisha unga wa ngano inahitaji umeme mwingi, endapo umeme unakatika inakuwa vigumu  kutumia jenereta kutokana na gharama kuwa kubwa,” anafafanua.

Alipoulizwa kama wanapata umeme wa uhakika alijibu: “Kipindi cha kiangazi huwa tunapata tatizo kubwa la umeme hapa kiwandani kwetu. Huenda  ni kwa sababu kipindi hiki mabwawa mengi ya kuzalisha umeme na haswa Mtera yanakuwa hayana maji ya kutosha na hivyo umeme unaozalishwa kuwa mdogo,” anasema.

Anasema kipindi cha kiangazi uzalishaji hupungua na hushindwa kukidhi mahitaji ya baadhi ya wateja wao.

“Katika kipindi hiki uzalishaji hushuka kwa asilimia 20. Hata hivyo, mwaka huu kumekuwa na unafuu mkubwa katika upatikanaji wa umeme ukulinganisha na miaka ya nyuma,” anaeleza.

Kampuni ya Tan Dairies Limited ya jijini Dar es Salaam inayozalisha maziwa ya Desa, ni moja ya kampuni  ambayo uzalishaji wake unategemea sana umeme wa Tanesco.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda  hicho, Simon Swai, anasema ukosefu wa umeme wa uhakika katika hatua mbalimbali za uzalishaji wa maziwa  umesababisha  gharama za uzalishaji kuongezeka  na kuisababishia kampuni hasara.

“Maziwa ni zao linalohitaji uangalizi wa hali ya juu  mara tu linapotoka kwa ng’ombe. Maziwa yanapokamuliwa  yanahitaji kuhifadhiwa katika  joto maalumu ambalo vijidudu (bacteria) hawataweza kuingia na kuyaharibu.

“Wakati tunapokuwa kwenye uzalishaji, mara nyingine umeme hukatika ghafla na tunakuwa hatujajiandaa. Umeme unapokatika maziwa yaliyokuwa kwenye uzalishaji huharibika na hata kama yakitoka salama hayawezi kuwa na  ubora unaotakiwa na  tunalazimika kuyamwaga na hivyo kutusababishia hasara,” anaeleza.

Anasema kampuni yake hukusanya maziwa  vijijini kutoka kwa wafugaji.  “Vituo vyetu vya kukusanya maziwa vina uwezo wa kukusanya lita 2000 hadi 3000. Nishati ya umeme inahitajika kwa ajili ya kuyahifadhi maziwa hayo yasiharibike. Katika vituo viwili vya Dumila na Kilosa tunalazimika kuwa na majenereta ya dharura  ambayo  uendeshaji wake ni gharama. Kwa mfano,  tangu Januari mpaka sasa tumetumia Sh milioni 2.9 kwenye vituo hivyo viwili pekee kwa ajili ya mafuta ya jenereta,  gharama ambazo zingeweza kuepukwa endapo kungekuwa na umeme wa uhakika,” anafafanua  bila kusema wanalipa kiasi gani kwa Tanesco kwa mwezi.

Swai anabainisha kuwa, matumizi ya jenereta kupoza maziwa yakiharibika  yanafanya bidhaa hiyo kutokuwa na ubora kwa sababu  huchelewa kupoza na kufanya kiwango cha kuchachuka kivuke kipimo kinachotakiwa.

“Gharama tunayoibeba ni zaidi ya hapa kiwandani. Tunapompelekea mlaji nako kuna tatizo kwa sababu maduka mengi hayana jenereta kwa ajili  ya dharura. Mlaji anapokuja kununua akakuta bidhaa haipo katika ubora wake au zimeharibika kutokana na kukatika kwa umeme. Ili tuendelee kufanya biashara na huyu mtu, ni lazima tuchukue bidhaa mbovu na kumpa nyingine nzuri kwa vile biashara ni ya ushindani na tusingependa kumpoteza mteja,” anaeleza kwa masikitiko.

“Kiwanda hiki kinatumia umeme wa njia tatu. Tunazo laini tatu na mashine zinaendeshwa na laini zote tatu. Kitu kinachotugharimu kwamba  wakati uzalishaji unaendelea, utakuta umeme unakatika kwenye laini moja au unakatika mara kwa mara na kurejea na kusababisha  kompresa zetu  kuungua.

“Tatizo hili linapotokea mara kwa mara husababisha hasara. Kwa mfano, mwaka huu tumeshatumia Sh milioni 15.9 kwa ajili ya kutengeneza mashine. Pamoja na kwamba tumeweka vifaa vya kurekebisha umeme unaoingia  lakini  bado tatizo lipo,” anaeleza.

“Bahati mbaya katika nchi yetu hatuna mashamba mengi na makubwa   ambayo  yana uwezo wa  kulisha viwanda vya maziwa. Bado tunategemea wafugaji wadogo wadogo ambao wapo vijijini. Ukosefu wa umeme wa uhakika vijini ni moja kati ya sababu zinazofanya tushindwe kuwekeza na kupanuka zaidi,” anasema.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umeonyesha kuwa si viwanda vya maziwa tu vinavyoathiriwa na umeme. Kama ilivyo kwa baadhi ya mikoa hapa nchini, ukosefu wa umeme wa uhakika umekuwa ni changamoto kwa viwanda mkoani Morogoro  na Tanga.

Meneja utumishi na utawala wa kiwanda cha nguo cha 21st  Century  kilichopo  Kihonda Manispaa  ya Morogoro,  Flotentine Mbaga, anasema kiwanda hicho kimekuwa chachu ya kuongeza ajira kwa vijana lakini uzalishaji umekuwa ukiathiriwa na ukosefu wa umeme wa uhakika.

“Kutokana na kilichotokea kwenye gridi wakati umeme unapokatika au kucheza (flactuation), hasara inayotokea kutokana na mashine kuharibika ni kubwa. Kwa mfano Novemba 14 mwaka jana, umeme ulirudishwa kiwandani saa 3 usiku baada ya kukatika toka saa 3 asubuhi. Baada ya kuwasha mashine iligundulika kuwa pamoja na mashine nyingine nyingi zilizopata uharibifu mdogo, kuna kompresa  moja iliharibika na kugharimu kiwanda Sh milioni 80 kutengeneza,” anaeleza.

Akaongeza : “Umeme unapokatika kiwanda kinapoteza mapato ya Sh milioni 5 kwa saa. Pia kuna gharama nyingine zinazotokea umeme unapokatika, kwa mfano kati ya August na Desemba 2014, kiwanda kilipoteza zaidi ya Sh milioni 270, ikiwa ni nguo, madawa na vyakula vilivyoharibika.”

Mbaraka Ahmad kutoka Kiwanda cha kutengeneza mikate cha Baraka Bakery kilichopo Msamvu mjini Morogoro, anasema kukatikakatika kwa umeme wakati wakiwa katikati ya uzalishaji kumekuwa kukiwasababishia hasara kubwa na isiyo ya lazima.

“Umeme unapokatika tunalazimika kununua lita 30 za mafuta kwa ajili ya kuendeshea jenereta, gharama ambazo zingeweza kuepukika kama kungekuwa na umeme wa uhakika,” anaeleza

Mbaraka.

Anasema ni muhimu kwa Tanesco kutoa taarifa wakati  wanapotaka kukata umeme  na wanapokata umeme ili kuepusha hasara zinazoweza kuzuilika kwa sababu umeme unapokatika bila taarifa na kurudi kwa kasi, husababisha mitambo kuungua na bidhaa zinazotengenezwa kuharibika.

Hata hivyo, katika jitihada za kuifanya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika, Wizara ya Nishati na madini imetenga asilimia 94 ya bajeti yake ya mwaka huu wa fedha kwa maendeleo ikiwamo miradi ya umeme.

Kule Tanga Kiwanda cha Tanga Cement kimezima kinu kimoja baada ya kuzindua kinu kipya, kwani umeme uliopo hautoshelezi kuendesha kinu cha ziada na hivyo kuomba waongezewe umeme kwa miezi sita iliyopita  bila mafanikio.

Kwa kifupi hali ni mbaya, umeme hautoshi nchini na Serikali itumie sekta binafsi na si kuwanyanyapaa kama inavyofanya kwani itakuwa shida kufikia malengo bila wao.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amewahi kunukuliwa akisema kuwa, ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa ikizalisha megawati 10,000 za umeme kutoka megawati 1,500 zinazozalishwa kwa sasa, bila ya kuainisha  atafikiaje lengo hili na hivyo kuaminika ni kuwa alinacha  au ni porojo za kisiasa kwa kusema watu wanayotaka kusikia  na bila  kutekeleza chochote kwani hakuna kinachoshindwa na mdomo.

Anasema hatua hiyo itasaidia nchi kuwa ya viwanda kwani kufikia muda huo, kila Mtanzania ataweza kupata uniti 3,000 za umeme kwa mwaka kutoka uniti 130 za sasa. Yakitokea ni habari njema kwa watu na uchumi wa  nchi hii. Tusubiri ingawa  hakuna mipango!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles