26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Watanzania waanza kunufaika JNHPP

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said amesema kuwa mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) umeanza kuwanufaisha Watanzania hata kabla ya kukamilika.

Hayo yaliyasema jana alipofanya mahojiano na mwandishi wa habari hii kuhusu ziara ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali waliyoifanya Juni 20, mwaka huu kukagua maendeleo ya mradi huo ulioko Rufiji mkoani Pwani.

Zena ameyataja mafanikio hayo kuwa ni ajira kwa Watanzania pamoja na matumizi ya malighafi za ndani ya nchi katika ujenzi wa mradi husika.

Alisema kuwa ujumbe huo ulifurahishwa kujionea kwamba asilimia kubwa ya wafanyakazi walioko katika mradi huo ni Watanzania. 

Aidha, walifurahishwa kuona kuwa malighafi zinazotumika zinatoka Tanzania.

“Nchi yetu imeanza kunufaika kabla mradi huu haujakamilika, hususan katika upande wa wafanyakazi na malighafi. Kwahiyo uchumi umeanza kukua katika hatua hii ya utekelezaji wa mradi,” alisema Zena. 

Aliongeza kuwa mradi utakapokamilika, Serikali inatarajia kupata umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu ambao utasaidia zaidi katika kuendesha viwanda vilivyopo pamoja na kuhamasisha vingine vije kuwekeza.

Zena amemshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kutenga fedha za ndani kutekeleza miradi ya kimkakati, ukiwemo huo wa Julius Nyerere.

Alisema JNHPP ni miradi ambao utaipeleka nchi yetu mbele.

Akizungumzia manufaa zaidi yatakayopatikana baada ya ujenzi wa bwawa katika mradi husika kukamilika, alisema kuwa nchi itaingia kwenye ramani siyo tu ya Afrik,a bali pia ya dunia ikiwa ni miongoni mwa nchi zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme wa uhakika.

Awali akizungumza baada ya ziara hiyo, kiongozi wa msafara, Profesa Sifuni Mchome, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, alipongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo, akisema wameridhishwa na kufurahishwa na maendeleo yake.

“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu John Pombe Magufuli kwa maono haya makubwa ambayo tunaamini yatakapokamilika taifa litakuwa limefunguka na kazi mbalimbali zitakuwa zinaendelea kufanyika katika kujenga uchumi wetu, ili kufikia azma yetu ya uchumi wa kati ifikapo 2025,” alisema Profesa Mchome. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles