24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 25, 2022

Lukuvi aagiza ofisi za mikoa kutoa hati ndani ya siku saba

Na Amina Omari -Tanga

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameziagiza ofisi za ardhi za mikoa kutumia siku saba pekee kukamilisha mchakato wa hati na kuzigawa kwa wananchi.

Lukuvi alitoa agizo hilo jana wakati wa ufunguzi wa ofisi ya ardhi Mkoa wa Tanga.

Alisema kutokana na ofisi hiyo kuwa na mahitaji yote yanayohitajika, haoni sababu ya wananchi kuchelewa kupata hati zao.

Lukuvi alisema Serikali imeamua kusogeza ofisi karibu na wananchi ili kuhakikisha wanapata huduma haraka na kwa wakati bila  kutumia gharama za ziada.

“Kanda ya Kaskazini mlikuwa mnatumia gharama kubwa kufuata hati zenu Moshi, uwepo wa ofisi karibu na maeneo yenu utawezesha kupata huduma haraka,” alisema Lukuvi.

Alisema wananchi walikuwa wanalalamika gharama kubwa za umiliki wa ardhi, lakini gharama hizo zilikuwa kubwa kutokana na kufuatilia hati ofisi za kanda.

“Mkoa wa Tanga tumeweza kuleta hati 18,260 za wananchi ambazo walishindwa kuzichukuwa kule Moshi kutokana na gharama, tumeleta ramani za upimaji 540 na kumbukumbu za michoro ya zamani ya mkoa huu tangu  enzi ya ukoloni,” alisema Lukuvi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema tangu ofisi hiyo iwepo kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kulipa kodi.

“Changamoto pekee iliyobaki ni wenye mashamba makubwa ambao wanamiliki maeneo makubwa ya ardhi na kushindwa kuyaendeleza, tumeendelea kuwasihi warudishe hati kwako uweze kuzifuta na maeneo ya ardhi wagaiwe wananchi wenye uhitaji,” alisema Shigela.

Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Tanga, Tumaini Gwakisa alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja walichofanya kazi, hati 350 zimeshasajiliwa na kugaiwa kwa wananchi.

Alisema  michoro 41 yenye viwanja 16,484 imeidhinishwa ili kuendelea na taratibu nyingine za utoaji wa hati.

“Tumeweza kuendelea kukusanya maduhuli ya Serikali  ngazi za halmashauri. Juni pekee tumekusanya Sh milioni 929.8 kutoka kwa wadaiwa sugu wa kodi za ardhi,” alisema Gwakisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,160FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles