28.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

WATAKAOANDAMANA WATASIMULIA-JPM

Na JUDITH NYANGE -MWANZA


RAIS Dk. John Magufuli ametoa onyo kwa mtu yeyote atakayejaribu kuandamana kwa kusema watakaokaidi agizo hilo, kitakachowapata watasimulia.

Akizungumza jana, wakati wa sherehe za ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB wilayani Chato, mkoani Geita, Rais Magufuli alisema Watanzania wanapozungumza na kukaa kwa amani nchi nyingine hazifurahi, hivyo  akawasihi wananchi kutambua amani iliyopo nchini ni karaha kwa nchi nyingine na kuwa maendeleo yana vita kubwa.

“Wapo watu wangependa nchi hii tuwe na migogoro migogoro, wapo watu ambao wameshindwa kufanya siasa za kweli, wangependa kila siku tuwe barabarani tunaandamana.

“Watu wao wanahamia huku wao wanabaki wanaandamana kule, nimeshasema ngoja waandamane watakiona, kama kuna baba zao wanawatuma watakwenda kuwasimulia vizuri.

“Niliapa kwa Katiba kwamba nchi hii lazima iwe ya amani, nataka tujenge uchumi wa kweli, Watanzania watajirike, na hali ya Watanzania imeanza kwenda vizuri, mwanzo ni mgumu, lakini nataka niwaambie Watanzania tupo kwenye right track, tuvumiliane tufike mahali ambapo Tanzania hii iwe ni nchi ya asali,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliwataka pia Watanzania kuwa wazalendo na kwamba, wakati mwingine mambo yanapokuwa mazuri, wengine huchukia.

“Mnapokaa kwa amani, mnazungumza kwa amani, wakati nchi nyingine kila siku wanapigana msifikiri wanafurahi, kwanini Somalia kila siku wafe? Kwanini Libya vijana wanaamua kwenda wafe baharini, ili tu waende kwenye nchi za Ulaya, wakati Libya miaka ya nyuma hata mtu ukioa unapewa dola 50,000 leo Libya wanaikimbia.

“Ni lazima Watanzania mfikirie, mnapoona nchi kama Iraq wanapigana watu wanaenda kujaribishia mabomu yao na mizinga yao nchi iliyokuwa imekaa vizuri katika miaka ya nyuma, ni lazima Watanzania mjiulize.

“Amani yetu Wanzania ndiyo karaha kwa watu wengine, naomba Watanzania wote mkae mjifikirie mahali tulipotoka, mahali tulipo na mahali tunapokwenda.

“Maendeleo yana vita kubwa, ninyi wananchi wa Chato ni mashahidi, kwenye ‘genocide’ ya ndugu zetu Rwanda, Wanyarwanda walipotembea kwa miguu wengine mpaka Chato, wengine mpaka Mwanza, watu 1,000,000 walikufa, mnafahamu chanzo ni nini, redio zilichongea na baadhi ya makanisa yalihusika, lazima tujiulize,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza: “Nchi yetu inaenda vizuri sana, na mtu yeyote ukifanya kitu kizuri usifikiri watakupenda, kwanini upendwe? Hata ukiwa unafanya kazi popote, unajenga nyumba yako, unalima vizuri, unaweza kukuta majirani wanakuchukia, uzuri una gharama.

“Tunapoweza kujenga standard gauge kwa Sh trilioni 7.6 hela za ndani, msifikiri watu wanafurahi, tunapoamua kujenga Stigler’s Gorge ambayo itazalisha umeme zaidi ya megawati 2,100, usifikiri wanaweza wakafurahi, tunapoweza kununua ndege kwa fedha zetu, kitu ambacho tulishindwa kwa miaka 50, usifikiri watu wanafurahi, tunapoweza kulipa mishahara tarehe 21 umeshalipa, usifikiri wengine wanafurahi,” alisema Rais Magufuli.

Polisi nao waonya

Kwa upande wake, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo  wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, alifanya mkutano na waandishi wa habari na kusema Jeshi hilo litafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kwa kadiri linavyoruhusiwa na sheria, kuhakikisha maandamano yanayohamasishwa kufanyika nchi nzima hayafanikiwi.

Alisema hivi karibuni kuna baadhi ya watu wamejitokeza kuanzisha makundi mtandaoni yanayojiita Revolution Tanzania kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram.

Alisema lengo la kuandaa maandamano hayo nchi nzima ni kuhamasisha vurugu (civil disorder), kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za nchi.

“Niweke wazi kuwa vitendo vyovyote vya kuhamasisha vurugu yenye lengo la kuitoa serikali iliyo madarakani ni uhaini na mtu yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo ni mhaini. Nitoe onyo kwa watu wote na vikundi vinavyoratibu vitendo hivi kwa njia mbalimbali, ikiwamo mitandao ya kijamii kuacha mara moja. Tutawakamata na tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria,” alisema Marijani.

Aliongeza kuwa, anaamini vijana wengi wametumbukia kwenye suala hilo kwa mkumbo, hivyo amewasihi wazazi na walezi kuwakanya vijana wao.

 

Inaendelea……………………….. Jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles