Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WADAU wa Maendeleo kutoka Sekta mbalimbali nchini wakiwamo Watafiti na Wataalamu katika nyanja tofauti wanatarajiwa kujifungia kwa siku mbili jijini Dodoma kwa lengo la kujadili kwa pamoja jinsi ya kuboresha maisha ya watanzania na Maendeleo ya Nchi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Jumanne Novemba 9, 2021,jijini Dodoma, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) anaeshughulikia Utafiti, Profesa Bernadeta Killian, amesema wadau hao wanatarajia kushiriki kongamano la tatu la utafiti kwa Maendeleo Jumuishi linalotarajiwa kufanyika Jijini Dodoma Novemba 11 na 12.
Naibu Makamu Mkuu huyo amesema lengo la kongamano hilo kuwaunganisha wadau wa Maendeleo kutoka sekta mbalimbali,watafiti na wataalamu katika nyanja mbalimbali ili kujadili kwa pamoja jinsi ya kuboresha maisha ya Watanzania na Maendeleo ya nchi.
Amesema Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo.
“Hii itakuwa ni fursa ya kuwafahamisha wadau kuhusu matokeo ya tafiti katika miradi mbalimbali iliyofanywa na Maprofesa wahadhiri wahadhiri na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam wanaonufaika na ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Vyuo Vikuu na Taasisi na Taasisi za Utafiti zipatazo 10 za Nchini Sweden,”amesema.
Amesema washiriki zaidi ya 300 wanatarajia kushiriki kongamano hilo kutoka ndani na nje ya Tanzania ikiwemo wataalamu wanadiplomasia, wabunge, watunga sera na wadau kutoka mashirika yasiyokiwa ya Kiserikali.
“Zaidi ya Makala 85 za kitaaluma zitawasilishwa na mihtasari 28 ya sera mbalimbali itajadiliwa Ndani ya siku hizo mbili za kongamano,”amesema.