26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wasio na vyoo Serengeti faini milioni 1

Na Malima Lubasha, Serengeti

Katibu Tawala wilayani Serengeti mkoani Mara, Cosmas Qamara ametoa siku 30 wananchi wote wilayani humo kuhakikisha wanajenga choo bora majumbani mwao, ambapo baada ya hapo mahakama inayotembea itapita kila kijiji kubaini waliokaidi na wataokapatikana na hatia watalipa faini ya Sh.milioni  moja au kifungo cha miezi 6 ama vyote  pamoja.

Qamara alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kebosongo, Kisangura na Kibeyo kwa nyakati tofauti katika kampeni ya nyumba kwa nyumba ya kuelemisha jamii madhara ya kutokuwa na choo bora inayoratibiwa na Shirika la AMREF ikilenga kuwajengea uelewa wananchi juu ya ujenzi na matumizi sahihi ya vyoo bora.

Alisema hadi sasa takwimu zinaonyesha wenye vyoo wilayani humo ni asilimia 56 tu huku kukiwa bado kuna idadi kubwa ya wasiokuwa na vyoo hivyo baada ya siku 30 msako utafanyika kubaini waliokaidi maagizo ya serikali kuhusu usafi wa mazingira yaliyotolewa mwaka jana yanayoitaka kila kaya kuwa na choo bora.

“Tabia ya kutokuwa na vyoo ma kuendekeza kujisaidia ovyo vichakani ni changamoto inayochangia maji taka kutiririka katika vyanzo vya maji wakati wa mvua na kuhatarisha afya zatu na baadaye kusababisha kutumia gharama kubwa za matibabu.

“Sisi kama viongozi wenu tumeamua kuzungumza nanyi kuunga mkono kampeni hii ikiwa ni mwendelezo wa kufuatia maagizo ya serikali yaliyotolewa awali yanayoitaka kila kaya nchi nzima kuwa na choo ili kuepuka magonjwa kama kipindupindu, kuhara, na homa ya matumbo yanayotokana na uchafuzi wa mazingira,” alisema Qamara.

Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk. Emiliana Donald, alisema suala la watu kupuuza kujenga choo si jambo la kufumbia macho kwani kitendo hicho kinachangia idadi kubwa ya wagonjwa walioathirika na magonjwa ya mlipuko  hasa wakiwa watoto ma watu wazima.

Dk.Emiliana aliwataka wananchi kutopuuza suala la usafi wa mazingira na kuwaomba wakazi wa vijiji hivyo  kushiriki kuharibu mazalia yote ya mbu kuzunguka makazi yao na  kutumia chandarua ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria na pia aliwahimiza kujiunga  na mfuko wa Bima ya Jamii (CHF) ili kupunguza gharama za matibabu.

Wakizungumzia sababu ya kukosa  vyoo baadhi ya wananchi walidai ardhi yao inatitia chini kila wanapoandaa choo maelezo ambayo serikali ya wilaya ilikataa kukubaliana nayo na kusisitiza kukosa choo ni uzembe ambapo Kamanda Mkuu wa Polisi Wilayani hapa, Mathew Mgema aliwekea mkazo agizo hilo na kusema sheria ndogo za halmashauri na nchi zitatumika kuwatia hatiani watakaokaidi agizo la kujenga choo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles