26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

WASHTAKIWA MENO YA TEMBO WASHTAKIWA UPYA

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM                  |                     


WATU 11 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi kwa kukutwa na vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh bilioni 4.5 wameachiwa na kushtakiwa upya ndani ya masaa matatu.

Washtakiwa hao waliachiwa na kukamatwa upya jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, lakini walipandishwa kizimbani tena mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizire.

Wakili wa Serikali, Salim Msemo, aliwataja washtakiwa hao  kuwa ni Ally Shariff na Fatoumata Saumaolo, raia wa Guinea, Victor Mawalla, Calist Mawalla, Solomoni Kuhembe, Haruna Abdallah ‘Kasa’, Abas Hassan ‘Jabu’, Ismail Kasa, Khalfan Kahengela, Musa Ligagabile na Kassim Said@Bedui Alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Aprili 6, 2016 hadi 23 Juni, 2016  Dar es Salaam, waliratibu na kusafirisha vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya USD 2,105, 181, ambavyo ni sawa na Sh bilioni 4.5, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume cha sheria ya wanyama pori.

Alidai katika shtaka la pili kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao walijihusisha na nyara za Serikali kinyume cha sheria ya wanyamapori ambako Juni 23 mwaka juzi  jijini  Dar es Salaam walisafirisha vipande hivyo.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa watano kati ya hao, Ally, Victor, Calist, Haruna na Abbas wanadaiwa kuwa   walikutwa na vipande vya meno ya tembo  kinyume cha sheria za wanyamapori.

Upande wa Mashtaka alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote, kwa madai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo.

Hata hivyo, washtakiwa hao walilalamika mahakamani hapo kuwa hiyo siyo kesi mpya, ilifutwa saa tatu kabla hawajafunguliwa kesi hiyo mpya, hivyo waliomba kutendewa haki kwa sababu wanaumia gerezani na upande wa mashtaka unaumiza familia zao.

Hivyo waliomba hiyo kesi iende Mahakama Kuu kwa sababu hapo hawawezi kupata haki.

Wapo ndani tangu mwaka 2016 wakitaka kuomba dhamana Mahakama Kuu Upande wa Mashtaka unawaeleza kesi imeiva, wanahisi wanataka kuwaua.

Baada ya kusikiliza malalamiko, Hakimu Rwizire aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 3, 2018, kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles