Na BADI MCHOMOLO-DAR ES SALAAM
MCHEZO wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliowakutanisha watani wa jadi, Simba dhidi Yanga, ulichezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na timu hizo kutoka bila kufungana.
Matokeo hayo hayakudhaniwa na baadhi ya mashabiki hasa kutokana na tambo mbalimbali za wiki chache kabla ya hatima ya mchezo huo, kila upande wa mashabiki walikuwa wanavutia kwao kwa kuamini wanaweza kushinda.
Mchezo huo ulikuwa na ushindani nje na ndani ya uwanja, lakini matokeo yalikuja kujulikana baada ya dakika 90. Kulikuwa na sababu mbalimbali ambazo zilifanya timu hizo kutoshana nguvu bila ya kujali ubora wao.
Safu ya ulinzi
Kwa upande wa Simba ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo, walikuwa bora katika safu hiyo ambayo ilikuwa inaongozwa na beki wao wa kati, Erasto Nyoni, akisaidiana na Pascal Wawa, wakati huo beki wa kulia akicheza Shomari Kapombe, huku kushoto akicheza Mohamed Hussein.
Wawa hakuwa bora sana, lakini udhaifu wake ulikuwa unafichwa na Nyoni ambaye alikuwa bora katika idara yake, wakati huo Kapombe na Hussein wote wakitekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kilichowafanya Simba kuonekana kuwa bora katika safu hiyo ni kutokana na Yanga kukosa shinikizo la nguvu kwa washambuliaji wao, hivyo walinzi wa Simba walikuwa wanapata muda mwingi wa kupumzika.
Kwa upande wa Yanga wao walikuwa makini kwa kuwa walijua ubora wa washambuliaji wa wapinzani wao, hivyo walikuwa na maelewano mazuri kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yao na kuweza kuwazuia washambuliaji tishio wa Simba kama vile Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na Midie Kagere.
Idara ya kiungo
Simba walionekana kuutawala mchezo huo kwa asilimia kubwa katika dakika zote 90, ni kutokana na ubora wa safu ya kiungo. Mpira mwingi ulionekana kutawaliwa na nyota wa Simba ambao ni Jonas Mkude, James Kotei pamoja na Clatous Chama.
Kazi kubwa ya Mkude na Kotei ilikuwa ni kuhakikisha wanaunganisha mawasiliano kati ya walinzi na washambuliaji ikiwa ni pamoja na kuwazuia wapinzani wasiweze kutumia eneo la katikati, hapo waliweza kufanikiwa huku Chama akipokea mipira kutoka kwao na kuwapelekea washambuliaji.
Kwa upande wa Yanga viungo wao walikuwa na wakati mgumu katika eneo la katikati, kwa asilimia kubwa walizidiwa, mbali na nyota wao, Papy Tshishimbi, kujaribu kupambana lakini hakuweza kutakata kama wengi walivyodhani.
Alijaribu kushirikiana vizuri na kiungo mwenzake, Feisal Salum (Fei Toto), lakini walikuwa chini ya uangalizi wa hali ya juu, hivyo hawakuweza kuunganisha vizuri safu yao ya ushambuliaji.
Washambuliaji
Siku zote sehemu hii ni muhimu katika kuleta matokeo ya mchezo husika, lakini hapa ndipo sehemu kubwa ambapo pametupiwa lawama kwa kiasi kikubwa katika kila timu kwenye mchezo huo wa juzi.
Kutokana na Yanga kubanwa katika sehemu ya kiungo, hivyo walitengeneza nafasi chache katika lango la Simba, lakini nafasi hizo zilikuwa za hatari, moja akiipata beki wao wa pembeni, Gadiel Michael na nyingine akipata Tshishimbi.
Hizo ni nafasi mbili ambazo wachezaji hao walikosa umakini, lakini kama wangekuwa makini zingeweza kupeleka kilio pale Msimbazi.
Kwa upande wa Simba, wao walikuwa na kila sababu ya kushinda mchezo huo kama wangekuwa makini, kwa asilimia kubwa walifika lango la wapinzani zaidi ya mara sita kwa mipira ya hatari, lakini walikosa umakini.
Mshambuliaji Kichuya alikuwa wa kwanza kupata nafasi ya wazi akiwa yeye na mlinda mlango wa Yanga, Beno Kakolanya, lakini Kichuya hakuwa na utulivu na kujikuta akipaisha mpira juu katika dakika ya 21. Hata hivyo, dakika ya 41, Kagere alikosa nafasi ya wazi kwa kukosa umakini.
Baada ya dakika 45 kumalizika Simba waliamini kuwa watakuja na umakini baada ya kushindwa kufanya hivyo katika kipindi cha kwanza, lakini bado homa ilikuwa ile ile, dakika nne baada ya kipindi cha pili kuanza, beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe, alikosa bao la wazi akiwa yeye na kipa baada ya kupokea pasi kutoka kwa Kichuya.
Mbali na Simba kufanya mabadiliko katika safu ya ushambuliaji, lakini mabadiliko hayo hayakuwa na faida yoyote kwao, aliingia Saidi Ndemla kuchukua nafasi ya Chama, hata hivyo katika dakika ya 86, mchezaji huyo alikosa bao la wazi.
Japokuwa Yanga walikuwa na wakati mgumu kwenye mchezo huo, lakini sifa za pekee ziende kwa kipa wao Kakolanya, ambaye alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu, karibu mipira yote ya hatari ambayo ilikuwa inawainua mashabiki wa Simba kwa kuamini kuwa litakuwa bao alikuwa anaicheza.
Kwa upande mwingine kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alifanikiwa katika kuhakikisha timu yake inatoka na pointi, alijua kwamba Simba wapo kwenye kiwango cha hali ya juu, hivyo hakutaka kuwaruhusu wachezaji wake wacheze mpira wa kufunguka kama walivyofanya Simba.
Kama Yanga wangecheza kwa kuwafuatisha Simba, basi kungekuwa na uwezekano mkubwa wa Simba kuibuka na pointi tatu, lakini Zahera aliliona hilo na kuamua washambulie kwa kushtukiza na muda mwingi walinde lango, hivyo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa aliweza kupaki basi na kuwafanya wapinzani wasipate bao, ila timu zote zilikosa umakini.