BUJUMBURA, BURUNDI
WAPIGAKURA nchini hapa, jana walipanga mistari kupiga kura ya uamuzi iliyopania kuongeza muhula wa rais kutoka miaka mitano hadi saba.
Marekebisho hayo ya Katiba yakiidhinishwa, huenda Rais Pierre Nkurunziza akaongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.
Lakini kampeni hizo zimechafuliwa na tishio la upinzani kususia mchakato huo na uwapo wa madai kuwa Serikali imekuwa ikiwatisha wafuasi wa upinzani.
Umoja wa Mataifa (UN) unahofia huenda ghasia zikazuka baada ya mauaji ya watu 26 hivi karibuni.
Wiki iliyopita, washambuliaji ambao Serikali imewataja kuwa magaidi, walivamia Jiji la Chibitoke, wakafanya mauaji ya kiholela na kuaminika kutorokea taifa jirani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Serikali inaamini walikuwa wanajaribu kuvuruga kura hiyo ya uamuzi kwa kutia watu hofu ili wasijitokeze.
Rais Nkurunziza amekuwa akipiga kampeni, akiwataka wananchi kuamini kuwa katiba hii mpya ni ya manufaa kwao.
Lakini wanaopinga wanamwona rais kama aliye na tamaa ya kung’angania uongozi.
Aidha wapinzani wake wanamshutumu kwa kupuuza makubaliano yaliyoafikiwa Arusha, Tanzania, ambayo yaliweka muda wa kuwa rais usizidi miaka 10.