24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

NATALIYA KUZNETSOVA: MWANAMKE MWENYE MISULI KULIKO WOTE DUNIANI

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA


AKIFAHAMIKA kama mwanamke mwenye misuli zaidi duniani, Nataliya Kuznetsova anatisha si mchezo katika ulimwengu wa utunishaji misuli.

Misuli yake mikubwa ya kutisha inawafanya hata baadhi ya watunisha misuli wa kiume wanapokutana mbele yake kujiona wadogo kama piriton.

Lakini pia kama wanyanyua vitu vizito wote, Nataliya hakuwa na mwili uliotuna kiasi hicho. Aliwahi kuwa mwembamba, wa kawaida, msichana kama wengine.

Akichukizwa na mabezo na kutaniwa alikokutana nako mitaani kutokana na wembamba wake na mwili usio kakamavu, mrembo huyu akasaka namna ya kuondokana na hali hiyo.

Katika umri wa miaka 14, aliamua kujiunga na kituo cha kunyanyua vitu vizito (Gym) ili kujiongezea misuli.

Alianza kama utani na kujikuta akitokea kunogewa nao na hivyo kwenda gym kila siku na mabadiliko ya haraka ya mwili aliyoshuhudia yalimfurahisha.

Katika umri wa miaka 16, miaka miwili tangu ajiunge na gym, tayari akawa bingwa wa mashindano ya unyanyuaji vitu vizito katika mkoa wao.

Sasa, Nataliya (26) ana mwili mkubwa wa kutisha na kibabe na katika urefu wake wa futi 5. 5 ana mzingo wa inchi 13.5 wa msuli wake wa mkono wa ndani (bicep) na mzingo wa inchi 28.3 mguuni.

Mwaka 2014, Nataliya aliweka rekodi ya kunyanyua uzito wa lbs 529 sawa na kilo 239.95 na kunyanyua uzito kwa kulala katika bench (bench pressed) wa lbs  374 sawa na kilo 169.644 na kumfanya kuwa bingwa wa Ulaya anaoshikilia hadi sasa.

Natalia alianza mazoezi akiwa na uzito wa kilo chini ya 40 sasa ana uzito mkubwa wa kilo 90 na amepanga kusonga mbele.

Ni mzaliwa wa Chita, wilayani Chitinsky nchini Urusi aliyehitimu mwaka 2013 katika Chuo Kikuu cha Moscow State Academy of Physical Culture.

Ijapokuwa ujengaji wa miili umemtengenezea jina, si kila mtu yu shabiki wake.

Hupokea maelfu ya ujumbe mchafu na kuchukiza kutoka watu wasojulikana mitandaoni, ambao kamwe hawangedhubutu kuinua sauti kumtukana ana kwa ana! wakikosoa staili yake ya maisha na mwili.

Wakati wengine wakivutiwa naye na kumuona mfano wa kuigwa na kichocheo cha kweli cha mchezo huo, wengine wanamuona kama uchuro na kudhani kuwa ameharibu mwili wake.

Nataliya mwenyewe anajaribu kutoruhusu wamchukiao na kumbeza kumrudishe nyuma.

Lakini anakiri wakati mwingine inaumiza na alifikia wakati alisitisha kuandika mijadala kwa sababu alipokea kauli nyingi za kuchukiza.

Hata hivyo, huonekana katika mitandao ya jamii na ana maelfu ya wafuasi katika ukurasa wake wa Instagram, ambao hutoa kauli nzuri za kumtia moyo na kumuunga mkono.

Baada ya kutwaa vikombe mbalimbali akikosa mpinzani barani Ulaya, Natalia, ambaye ametajwa kuwa mwanamke mwenye misuli zaidi duniani na kuweka rekodi mbalimbali za dunia karibu 30 mwaka juzi alitangaza kustaafu.

Lakini Novemba mwaka jana, akatangaza kurudi tena katika mchezo huo, akisema ilikuwa mapema mno kuuacha.

Mbali ya kuinua vitu vizito, Natalia ameanza kutoa mafunzo kwa wengine ili kuwasaidia kutimiza ndoto zao.

Kuhusu umaarufu wake, anasema: “Watu hunitambua kirahisi, mwili wangu wa kimichezo huonekana kirahisi ndani ya mavazi nivaaayo. Watu wengi huniomba kupiga nami picha.”

Nataliya anakiri kwamba aliwahi kufikiria kutumia dawa za kuongeza homoni ili kukiuza misuli, lakini akaona kwamba hazimfai.

Anasema kwamba anaweza kufanya vyema na kuwa na umbo kamili bila kuzitumia, lakini alisisituiza baadhi ya dawa zilimsaidia kufanya vyema katika mashindano.

Bingwa huyo wa dunia ana bahati kwa vile katika mashindano aliyoshiriki hakuna lililokuja na wazo la kumtaka achukue vipimo iwapo anatumia dawa zilizopigwa marufuku.

Kuhusu faida ya kifedha anayopata, anasema hiyo ni ya gharama kuutunza mwili wake maana ili kumfanya aendelee kuwa fiti, mafunzo kila siku na kusafiri mara kwa mara fedha zinahitajika sana.

Hilo linamfanya mara nyingi asiwe na fedha kutokana na kukosa muda wa kufanya kazi nyingine zaidi ya kutumia muda mwingi gym.

Kwa sababu anategemea wafadhili zaidi ili kugharimia staili yake hiyo ya maisha.

Hata hivyo, kwa vile utunishaji misuli si maarufu sana Urusi kama ilivyo Marekani, ni kazi ngumu kupata wafadhili nchini humo na hivyo hujikuta akiwa na mzigo wa madeni.

Ili kukabili hilo amebuni njia ya kuongezea kipato ikiwamo kuwatoza kiasi kidogo cha fedha watu wanaotaka kuwasiliana naye katika mitandao ya jamii.

Nataliya ni mama wa mtoto mmoja na anaishi na mumewe mjini Moscow Urusi.

Hata hivyo, mrembo huyo mwaka 2015 aliwahi kukiri kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja baada ya kuishi muda mrefu bila mwanaume kutokaa na wanaume wengi kumuogopa.

“Kila mwanamke duniani ni mzuri siamini kuwa nikiwa mwanamichezo basi nitakosa mwanaume wa kunioa,” aliwahi kukaririwa akisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,051FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles