NYOTA wa mchezo wa tenisi nchini Uswisi, Stan Wawrinka, amejiondoa kushiriki michuano ya Olimpiki ambayo inatarajia kuanza kutimua vumbi kesho nchini Brazil.
Mchezaji huyo ambaye anashika nafasi ya nne kwa ubora wa tenisi kwa upande wa wanaume duniani, amejiondoa kushiriki mashindano hayo makubwa duniani baada ya kupata majeraha katika michuano ya Rogers Cup iliyofanyika huko Toronto nchini Canada.
Nyota huyu aliondolewa katika hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa na Kei Nishikori mwezi uliopita na kutokana na ushauri wa daktari wake ameamua kujiondoa katika michuano hiyo baada ya kuhisi maumivu.
“Nilikuwa na lengo la kuandika historia mpya katika michuano ya Olimpiki, lakini lengo langu haliwezi kukamilika kutokana na kusumbuliwa na maumivu, hivyo nimeona bora nijitoe katika michuano hiyo,” alisema Warrinka.
Wachezaji wengi mashuhuri wa mchezo huu wa tenisi wamejiondoa kushikiri michuano hiyo ikiwemo Roger Federer, Marcos Baghdatis, kutokana na kusumbuliwa na majeraha.